Wafia mgodini wakipora dhahabu

21Feb 2017
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
Wafia mgodini wakipora dhahabu

WATU wanne wamefariki dunia na idadi kama hiyo kujeruhiwa baada ya kufukiwa kwenye machimbo ya dhahabu eneo la Nanyuki, wilaya ya Chunya mkoani Mbeya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashari alisema ajali hiyo ilitokea jana asubuhi baada ya zaidi ya wanananchi 50 kuvamia shimo la dhahabu linalomilikiwa na Vincent Minja, mkazi wa jijini Dar es Salaam.

Kamanda Kidavashari alisema wananchi hao walivamia shimo hilo baada ya kupata taarifa kuwa linatoa dhahabu nyingi.

Hata hivyo, alisema wananchi hao walianza kuchimba bila kuchukua tahadhari, hali iliyosababisha shimo hilo kuporomoka na kuwafukia watu 11.

Kamanda Kidavashari aliwataja watu wanne waliofariki dunia ndani ya shimo hilo kuwa ni Andrew Paulo (26), Mark Frederick (22) na Isaack Mwanjale (30) wakazi wa kijiji cha Itumbi, na Hamis Mailosi (25), mkazi wa kijiji cha Mapogoro.

Aidha, aliwataja waliojeruhiwa katika tukio hilo kuwa ni Saimon Majaliwa (25), mkazi wa Itumbi, Mazoea Mahona (25), mkazi wa Mkoa wa Tabora, Benny Bahati (23), mkazi wa Kijiji cha Mapogoro na James Alinanuswe (26), mkazi wa Tukuyu wilayani Rungwe.

Alisema kilichosababisha shimo hilo kuporomoka ni wananchi hao kuchimba eneo hilo bila utaratibu na kwamba hawakuchukua tahadhari yoyote kutokana na hali ya mvua inayonyesha mara kwa mara.

“Wananchi wale tunawachukulia kuwa ni wezi kwa sababu walivamia eneo lenye leseni ya mtu mwingine. Taarifa za awali ni kwamba waliobainika kuwa wamefariki dunia ni wanne na wengine wanne wamejeruhiwa, lakini watatu walitoka wakiwa hai na walikimbia,” alisema Kamamda Kidavashari.

Alisema baada ya uokoaji, miili ya marehemu ilipelekwa kuhifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya huku majeruhi wakiwa wanaendelea kupatiwa matibabu hospitalini hapo.

Diwani wa Kata hiyo ya Matundasi, Kimo Chogga, alisema wananchi hao walianza kuvamia eneo hilo Jumatatu ya wiki iliyopita na kwamba walizuiliwa na mwenye leseni ya eneo hilo, lakini walikaidi.

Alisema ilipofika Alhamisi, walielimishwa vizuri na kukubali kusimamisha uchimbaji baada ya mwenye eneo kuwaeleza kuwa kufikia jana, atakuwa ameweka utaratibu mzuri wa namna ya kuchimba.

Hata hivyo, Chogga alisema wananchi hao jana asubuhi walivamia tena shimo moja wakidai mmiliki wa leseni ya eneo hilo naye aliendelea kuchimba.

Alisema baada ya kufukiwa, juhudi zilianza kufanyika za uokoaji na katika harakati hizo ndipo walipokuta watu wanne kati ya 11 waliokuwa wamefukiwa wameshafariki dunia, wanne wamejeruhiwa na wengine watatu walitoka wazima na kutoroka.

“Baada ya waliokuwa wamefukiwa kuokolewa, bado wananchi waliendelea kung’ang’ania waendelee kuchimba, hali iliyolifanya Jeshi la Polisi kuimarisha ulinzi na kuwataka wananchi hao waondoke waelekee ofisi ya kijiji kwa ajili ya mazungumzo," alisema Chogga.

Hata hivyo, alisema wananchi hao walianza kufanya fujo kwa kuzuia barabara kwa kutumia miba, magogo na mawe wakidai miili ya wenzao waliofariki dunia ili waendelee na maziko.

Nipashe lilimtafuta Mganga Mkuu wa wilaya hiyo, Dk. Stanford Mwakataghe, ili kuelezea hali ya majeruhi na miili iliyopokelewa katika Hospitali ya Wilaya, lakini simu yake ilikuwa haipokelewi.

Habari Kubwa