Wafuasi wa CHADEMA waachiwa

04May 2021
Lilian Lugakingira
Bukoba
Nipashe
Wafuasi wa CHADEMA waachiwa

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Bukoba imemwachia huru aliyekuwa Meya wa Manispaa ya Bukoba na mgombea ubunge Jimbo la Bukoba Mjini (CHADEMA), Chief Kalumuna na wafuasi wengine sita wa chama hicho waliokuwa wanakabiliwa na mashtaka manane likiwamo la kumjeruhi Mkuu wa Polisi Wilaya .....

ya Bukoba, SSP Babu Sanare.

Akisoma hukumu ya kesi hiyo namba 257 ya mwaka 2020 iliyokuwa inawakabili washtakiwa saba, hakimu wa mahakama hiyo, Joseph Ruambano, alitaja mashtaka mengine yaliyokuwa yakiwakabili washakiwa hao ni kusababisha vurugu na uharibifu wa mali.

Hakimu Ruambano alisema kuwa upande wa Jamuhuri walikuwa na mashahidi sita ambao walitoa ushahidi dhidi ya washtakiwa hao wakidai walitenda makosa hayo katika Uwanja wa Kaitaba kulipokuwa kunafanyika uapisho wa mawakala, wagombea wa udiwani na ubunge katika Jimbo la Bukoba Mjini.

Pamoja na washtakiwa hao kukubali kuwapo eneo la tukio siku hiyo, walikana kutenda makosa hayo kwa kuwa siku hiyo Uwanja wa Kaitaba kulikuwapo michezo ya wanafunzi, na timu ya Kagera Sugar ikifanya mazoezi, suala ambalo upande wa Jamhuri ulishindwa kuthibitisha kuwa wafuasi wa CHADEMA ndiyo waliohusika na tukio hilo.

Hakimu huyo pia alisema shahidi namba nne kwa upande wa Jamhuri SSP Babu Sanare aliyejeruhiwa wakati wa vurugu hizo, alishindwa kuthibitisha kujeruhiwa na mshtakiwa namba nne Audomalius Audax Joseph.

Naye mkuu wa mashtaka Mkoa wa Kagera, Basilius Yusuph, alisema kuwa wanaendelea kufuatilia hukumu hiyo, na kwamba wasiporidhika watakata rufani, huku wakili wa utetezi akidai kuridhika na maamuzi yaliyotolewa.

Wakili wa upande wa utetezi Lameck John alisema kuwa kesi hiyo ilifunguliwa kwa hisia, tu na kwamba ndiyo maana kila hoja imechambuliwa na kulikuwapo na kukinzana kwa upande wa ushahidi wa mashtaka.

Habari Kubwa