Wafungwa waliompora silaha askari, kumjeruhi wakamatwa

23Nov 2020
Francis Godwin
Iringa
Nipashe Jumapili
Wafungwa waliompora silaha askari, kumjeruhi wakamatwa

JESHI  la Polisi mkoani Iringa  limewakamata  wafungwa  wanne  wanaodaiwa kutoroka   baada  ya  kumshambulia kwa  mapanga  na  kumjeruhi  mwilini mlinzi, askari Magereza na kumpora silaha.

Wafungwa hao wanadaiwa kumpora  bunduki aina ya Uzi-gun yenye namba TZPS 5570-062974 Sajeni Feedolin  Madembwe  (53)  wa gereza la Iringa, mkazi wa Kibwabwa .

Kamanda  wa Polisi Mkoa wa Iringa, Juma  Bwire, alisema juzi kuwa tukio la wafungwa hao  kutoroka  lilitokea  Novemba 16, mwaka huu,   majira ya mchana  katika  msitu  wa Wilolesi,  Manispaa ya  Iringa,  wakati  askari  huyo  akiwasimamia  wafungwa kuchanja kuni kwa  ajili ya matumizi ya chakula  gerezani .

Aliwataja   wafungwa hao  waliokamatwa  kuwa ni Richard  Mbondamila (22) mkazi wa Imalutwa, Ilula  wilayani Kilolo  aliyekuwa  akitumikia  kifungo cha miaka mitano jela kwa  kosa la wizi,  Haroun  Boniphace (22)  mkazi wa Majengo Migoli  mkoani njombe  aliyekuwa  akitumikia  kifungo cha  miezi  saba kwa  kosa la  kujeruhi  wanyama.

Wengine ni Staford Kalinga (20)  mkazi wa Mtuwa  Ilula, wilayani Kilolo aliyekuwa  akitumikia  kifungo cha   kukutwa na bangi  na  Isack Kawogo (24) mkazi wa  Mgodini, Ramadhani mkoani Njombe aliyekuwa akitumikia kifungo cha miaka minane kwa kosa la kuvunja na kuiba .

Alisema  baada ya  kupata  taarifa  za kutoroka, Jeshi la Polisi  lilianza msako mkali na usiku wa Novemba 16  majira ya saa 4:00 usiku, waliwakamata Mbiondamila na Boniphace eneo la Gangilonga wakiwa katika  jitihada za  kutoroka  kwenda Iringa mjini. Pia alisema siku ya pili walimkamata Kalinga akiwa eneo la Ndiuka akijaribu kutoroka.

Kamanda  Bwire  alisema  usiku wa kuamkia  Novemba 20, Kawogo ambaye alikuwa akifahamika kwa  jina la kiuhalifu kama Mnyapara,  aliyepora  silaha ya askari magereza, alikamatwa akiwa  Njombe  na tarifa kamili  itatolewa na polisi mkoani humo.

Katika hatua nyingine, Kamanda Bwire alisema  jeshi   hilo  linajivunia mafanikio  makubwa  katika  kesi ya  ubakaji  baada ya mwaka 2018  kumkamata Akwino  Mtavangu  (36)  mfanyabiashara  mkazi wa Mafinga kwa tuhuma  za kubaka  mtoto  mwenye  umri wa  miaka sita, mwanafunzi wa darasa la kwanza (jina lake na shule vinahifadhiwa).

Mtavangu anadaiwa kuwa siku ya tukio, alimrubuni  mtoto   huyo akiwa anatoka  shuleni  na  kumpandisha kwenye pikipiki na kwenda naye  nyumbani  kwake kisha  kumbaka na kumficha  kwenye  nyumba ambayo  haijaisha.

Mtuhumiwa huyo alifikishwa mahakamani na Oktoba  19, mwaka huu, katika Mahakama ya  MKazi Mkoa wa Iringa, alikutwa na hatia na  kuhukumiwa  kifungo cha miaka  30 jela .

Habari Kubwa