Wafurahia mradi kilimo cha umwagiliaji

01Oct 2017
Marco Maduhu
Nipashe Jumapili
Wafurahia mradi kilimo cha umwagiliaji

WAKULIMA wa kijiji cha Nyida katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, wamefurahia mradi wa kilimo cha umwagiliaji ambao utawawezesha kulima na kupata mavuno mengi kwa uhakika.

Ujio wa mradi huo pia utawafanya kuondokana na janga la njaa pamoja na kukuza uchumi katika familia zao.

Mradi wa kilimo hicho cha umwagiliaji kijijini humo umefadhiliwa na serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Kimataifa la Misaada (Jica) na utakuwa na uwezo wa kumwagilia ekari 1,552.5 hivyo kuondokana na kilimo cha msimu ambacho hutegemea mvua.

Wakizungumza juzi wakati wa kukabidhiwa mradi huo, Ester Kibila na Sylvester Mhoja, kwa nyakati tofauti walisema mradi huo utakuwa mkombozi kwao kwa kuwa awali walijenga tuta kwenye Mto Tungu kwa ajili ya kutunza maji ya kumwagilia mashamba yao, jambo ambalo liligonga mwamba.

“Tunaishukuru serikali ya Japan kwa kutuletea mradi huu wa umwagiliaji kijijini kwetu, Hapa tuna Mto Tungu lakini kutokana na kutokuwa na utaalamu tulishindwa kuutumia ipasavyo lakini sasa baada ya kujengewa mtaro huu kitaalamu na kutunza maji mengi, utatusaidia kuondokana na kilimo cha msimu na kuinuka kiuchumi,” alisema Kibila.

Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Ngassa Mboje, aliyekuwa mgeni rasmi wakati wa uzinduzi huo, aliipongeza Japan na kuwasihi wakulima kuutunza na  kuutumia ipasavyo mradi huo kunufaika nao kwa kulima mazao ya chakula na biashara ili kuondokana na wimbi la umaskini.

Naye Mratibu wa Mradi huo kutoka Japan, Taira Kazufuni, alisema wamesaidia wanakijiji hao kama sehemu ya somo darasa ili halmashauri zingine ziige mfano huo na kuanzisha kilimo cha umwagiliaji.

Alisema mradi huo umegharimu  zaidi ya Sh. milioni 100 na utakuwa mfano mzuri wa kuigwa nchini kwa kuwa wataalamu mbalimbali watakwenda kujifunza na kuanzisha kwenye maeneo yao na hatimaye kukipa kisogo kilimo cha kutegemea mvua na kuwaondoa wananchi kwenye umaskini huku suala la njaa likibaki kuwa historia.