Wafutiwa matokeo kisa udanganyifu

16Jan 2022
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Wafutiwa matokeo kisa udanganyifu

BARAZA la Taifa la Mitihani (NECTA) limewafutia matokeo watahiniwa 214 katika mitihani ya darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne kwa hutuma za kufanya udanganyifu.

​​​​​​​Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde.

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Charles Msonde, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuhusu taarifa ya matokeo ya darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne kwa mwaka 2021.

Kwenye taarifa yake hiyo, Dk. Msonde alisema kati ya watahiniwa waliobainika kufanya udanganyifu, watahiniwa 83 ni wa darasa la nne, watahiniwa 27 ni kidato cha pili, wengine 102 ni kidato cha nne na wawili ni wa mtihani wa maarifa (QT).

Dk. Msonde alisema: "Baraza la Mitihani limefuta matokeo yote ya watahiniwa 214 waliofanya udanganyifu katika mtihani kwa mujibu wa kifungu cha 5(2)(i) na (j) cha Sheria ya Baraza la Mitihani Sura ya 107 kikisomwa pamoja na cha 30(2)(b) cha Kanuni za mitihani.

Kadhalika, Dk. Msonde alisema pia NACTE limezuia kutoa matokeo ya watahiniwa 555 ambao walipata matatizo ya kiafya na kushindwa kufanya mtihani kwa masomo yote au idadi kubwa ya masomo.

Alieleza kuwa watahiniwa hao wamepewa fursa ya kufanya mtihani kwa masomo ambayo hawakufanya kwa sababu ya ugonjwa kwa mwaka 2022 kwa mujibu wa kifungu vha 32(1) cha kanuni za mitihani.

Habari Kubwa