Wageni waanza kupimwa ebola

17May 2018
Lilian Lugakingira
BUKOBA
Nipashe
Wageni waanza kupimwa ebola

SERIKALI Kagera imeanza kuwapima watu wanaoingia kutoka nchi jirani kupitia mkoa huu, ili kubaini kama wana maambukizi ya ugonjwa wa ebola.

Hatua hiyo inafuatia kutangzwa kwa mlipuko wa ugonjwa huo kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Manispaa ya Bukoba jana, Kaimu Ofisa Afya Mkoa wa Kagera, Geraz Ishengoma alisema kuwa kila mgeni anayeingia nchini anapimwa na anayeonekana ana dalili zinazofanana na ugonjwa huo, hupelekwa kupimwa zaidi.

Ni mara ya pili katika mwaka mmoja kwa serikali kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya ebola. Mei 29, mwaka jana Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsi, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alisema wageni kutoka nchi hiyo wangesajiliwa na kufuatiliwa hadi wanakoishi ili kujiridhisha kama hawana virusi vya ebola.

Kaimu Ofisa Afya Mkoa wa Kagera, Ishengoma alisema jana: “Tumeweka kambi katika maeneo ya mpakani hasa Mutukula, Murongo, Kabanga na Rusumo, (na) kila mtu anayeingia anapimwa ikiwamo joto la mwili.

"Tunayekuwa na shaka naye, tunamtenga na kumchunguza zaidi.”

Alisema kuwa kambi hizo za mpakani ziliwekwa baada ya serikali kutangaza kuwapo kwa ugonjwa huo DRC Mei 8, mwaka huu, na kuwa hadi sasa hakuna mtu yeyote aliyebainika kuwa na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.

Alisema virusi vya ugonjwa huo vinaambukizwa kwa kugusa damu au majimaji, kugusa maiti ya mtu aliyekufa kwa ugonjwa huo na kugusa wanyama wenye maambukizi, na kuwa dalili zake huanza kuonekana kuanzia siku mbili hadi 21 tangu mtu anapoambukizwa.

Ishengoma alitaja dalili za ugonjwa huo kuwa ni homa kali, kulegea mwili, kichwa kuuma kunakoambatana na kutapika na kutokwa na damu sehemu tofauti za mwili, ikiwamo puani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu Salum Kijuu, alisema serikali imechukua kila tahadhari ili kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini kupitia mkoa wa Kagera.

“Kumbukeni Kagera ni mkoa ambao unapakana na nchi nyingi, zikiwamo za Rwanda, Burundi na Uganda, lakini pia unapakana na mkoa wa Kigoma ambao watu kutoka Congo hupitia katika mkoa huo na kuingia Kagera hasa kupitia eneo la Murusagamba,” alisema.

Kijuu aliwataka wananchi kutoa taarifa haraka endapo watabaini kuwapo kwa mtu mwenye dalili kama za ebola katika maeneo yao, ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa.

“Lakini pia wananchi hawapaswi kugusana na mgonjwa mfano kugusa mate, majimaji na damu, kuepuka kugusa maiti, kutochelewa kupata huduma na kuzingatia usafi wa mwili,” alisema.

Alisema kuwa serikali inaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali, ili kuhakikisha ugonjwa huo hauingii nchini.

WAGENI WOTE

Mei mwaka jana serikali ilisema ingepima na kufuatilia kubaini endapo wana virusi vya ebola wageni wote wanaoingia nchini kutokea DRC.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri Ummy alisema wageni kutoka nchi hiyo watasajiliwa na kuwafuatilia hadi wanakoishi ili kujiridhisha kama hawana virusi hivyo.

Alisema mfumo huo unafanywa katika vituo vyote vinavyopitishia wageni, ikiwa ni pamoja na kwenye viwanja vya ndege, mipakani na bandarini.

“Tumelazimika kufanya hivi si kuwanyanyapaa watu wanaotoka DRC, lakini kwa ajili ya usalama na tunaomba watuvumilie katika hilo," alisema waziri Ummy Mei 29, mwaka jana.

"Ugonjwa huu ni hatari sana, tunataka tuwe na uhakika kwa sababu mtu anaweza kupata virusi jana na akaja nchini kwetu, lakini si rahisi kumtambua kwa haraka.

"Kwa hiyo inabidi tufuatilie maendeleo yake anapokuwa tayari ameingia nchini kujiridhisha zaidi.

“Naomba watendaji wetu ambao wako katika vituo hivyo wasifanye kazi kwa mazoea, wafanye hili zoezi kwa ufanisi kuhakikisha hakuna mtu anayetoka DRC anapita bila kuchunguzwa na tunaomba waandishi wa habari mfanye uchunguzi wa ndani kubaini kama kuna wasimamizi wanazembea.

"Mnaweza mkajifanya mnatoka huko na nyie ili muone kama mtachunguzwa na kujaza fomu hiyo, maana si mnajua watu wanafanya kazi kwa mazoea?”

Alisema serikali ilikuwa imetumia Sh. bilioni 1.5 katika kudhibiti ugonjwa huo usiingie nchini kwa kuandaa timu ya wataalamu, kununua vifaa kinga na vya kutambua wagonjwa na kuimarisha mfumo wa kufuatilia wagonjwa pamoja na huduma nyingine.

Habari Kubwa