Wagombea 10 upinzani waenguliwa udiwani

21Sep 2021
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Wagombea 10 upinzani waenguliwa udiwani

WAGOMBEA 10 kutoka vyama vya upinzani, wameenguliwa kuwania udiwani wa Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, kwa madai ya kukosa sifa.

Msimamizi wa uchaguzi huo mdogo wa Kata ya Ndembezi, Manispaa ya Shinyanga, Timothy Andrew, akizungumza jana na waandishi wa habari, alisema baadhi ya wagombea wa vyama hivyo vya upinzani, hawakukidhi vigezo vya kugombea udiwani, huku wengine wakishindwa kurudisha fomu.

Aliwataja wagombea walioenguliwa kuwa ni Abdala Sube kutoka Chama cha Demokrasia Makini, Rehema Mjengi (ACD), Antony Ndinda (SAU), Ramla Shija (NLD), Fatuma Ally (UMD), Emiliana Malema (CCK), Ibrahim Juma (CHAUMA), Lwitakubi Kabugulu (NRA), Amen Isangi (DP) na Mvano Idd, ACT-Wazalendo.

Pia alimtaja mgombea aliyekidhi vigezo vya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kupitishwa kugombea udiwani kata hiyo kuwa ni Victor Mmanywa kutoka CCM.

“Baada ya kikao kukaa na kumpitisha mgombea wa CCM, na kuwaengua wagombea wengine walikosa vigezo, kinachofuata ni zamu ya wananchi kuleta mapingamizi, ili tuendelee na hatua zingine za uchaguzi,” alisema Andrew.

Sababu ya kuengeliwa mgombea wa ACT-Wazalendo aliyekuwa ameteuliwa rasmi na kupewa barua ya uteuzi imeelezwa kuwa hakujaza  fomu namba 8 (c) na namba 10 (c) na kuzirudisha NEC kwa wakati.

Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Katibu Mwenezi wa chama hicho Jimbo la Shinyanga mjini, Omary Gindu, alisema mgombea wao alikuwa tayari amepewa barua ya uteuzi na kwamba mgombea wa CCM alimuwekeza pingamizi kwamba hakujaza fomu hizo kwa usahihi.

Kutokana na hatua hiyo, chama hicho kimesema kinajiandaa kukata rufani ngazi ya jimbo na nakala kuipeleka NEC ili kupata haki yao.

Naye mmoja wa wagombea udiwani ambaye ameenguliwa kwenye kinyang’anyiro hicho, Abdalla Sube, alikiri kuchelewa kurudisha fomu kwa maelezo kuwa gari alilokuwa amepanda akitokea Ushetu wilayani Kahama kuja Shinyanga mjini kupata matatizo njiani.

Uchaguzi huo mdogo katika Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, unafanyika kufuatia kifo cha aliyekuwa Diwani wa kata hiyo, David Nkulila, ambaye alikuwa Meya wa Manispaa ya Shinyanga, aliyefariki dunia Agosti, mwaka huu kwa maradhi ya moyo.