Wagombea wote waliochaguliwa kwa rushwa kukatwa- Samia

09Aug 2020
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Wagombea wote waliochaguliwa kwa rushwa kukatwa- Samia

MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan amesema Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika mchakato wake wa kuchambua wagombea waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali watatumia usemi wa Rais John Magufuli wa kukata wagombea wote waliochaguliwa kwa rushwa.

MAKAMU wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Aidha ameitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)  kuhakikisha  viongozi watakaochaguliwa hawatokani na rushwa.

Akifungua jengo la Ofisi ya TAKUKURU Wilaya ya Mpwapwa Jijini Dodoma jana amesema matukio ya rushwa sio ya kiungwana na ni uvunjaji wa Sheria na kurudisha nyuma maendeleo ya nchi.

"Sisi CCM tunaendelea na mchakato wa kuchambua wagombea waliojitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi,watakaobainika kuwa walijihusisha na vitendo vya rushwa tutawakata na kuwaengua kwenye mchakato huo,mheshimiwa Rais ana msemo wake tutawakata,tutautumia,"amesema Makamu wa Rais.

Amesema mgombea anayetoa rushwa ili achaguliwe hatotumia muda wa uongozi kuwahudumia Wananchi Ili wapate maendeleo bali atatumia dhamana a uongozi kurejesha fedha alizotoa kama rushwa wakati wa uchaguzi na pengine kujipatia fedha zaidi.

Amewataka Takukuru kuendelea kung'ata baadhi ya watendaji wake wanaochafua taswira hiyo na kusema amefurahishwa na hatua ambayo Takukuru wameanza nayo ya kung'ata waliohusika na ubadhirifu wa majengo manne ya Ofisi zake.

Habari Kubwa