Wagonjwa wa sikoseli wahitaji wakuu wa damu

02Jun 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Wagonjwa wa sikoseli wahitaji wakuu wa damu

Katika wiki mbili za maadhimisho na kuelekea kilele cha siku ya wachangia damu duniani,imeelezwa kuwa kuna  uhitaji wa damu kwa wagonjwa wa sikoseli mbali na makundi yaliyozoeleka ikiwemo wakina mama wanajifungua na watu mbalimbali ambao wamekuwa wakifanyiwa upasuaji.

Maadhimisho hayo yalioanza Juni 1,2020 ambapo kilele chake ni Juni 14 mwaka huu, yatatumika kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala ya uchangiaji damu na faida zake pamoja na kuwashukuru watu wanaojitolea kuchagia damu.

Mwenyekiti wa Desks and Chair Foundation, Sibtain Meghjee ndio aliyetoa maelezo hayo jana wakati akikabidhi msaada wa kanga, tisheti na trei za plastiki kwa uongozi wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama kituo cha Kanda ya Ziwa kilichopo Mkoani Mwanza, ikiwa ni sehemu ya kuthamini na kutambua mchango wa wadau wanaojitokeza kuchangia damu.

Meghjee, amesema kitengo cha damu salama kimekuwa na uhaba wa damu kutokana shule na vyuo kufungwa kutokana na janga la corona kwani wachangiaji wa damu kwa sehemu kubwa nchini ni wanafunzi wakifuatiwa na makundi mengine huku kundi linalohitaji damu zaidi ni watu wenye matatizo ya sikoseli.

Amesema wachangia damu wamekuwa mstari wa mbele mwaka mzima hivyo wao kama Desks and Chair Foundation  wameamua kutumia wiki mbili za maadhimisho kutoa shukrani kwa watu wote waliojitokeza katika kuchagia dau.

"Kwa leo hii kwenye kitengo cha damu salama tumekabidhi jozi 200 za kanga,tumechapisha tisheti 340 ambazo zina ujumbe na kauli mbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inayosema "damu salama ina okoa maisha",ambapo wachangiaji wa damu watakuwa wanapewa kama kumbukumbu pamoja na trei ambazo ni kwa ajili ya kuhifadhia vitu watakavyo pewa wachangiaji hao,nachukua nafasi hi kuwapongeza na kuwashukuru wachangiaji wa damu wote na tumeanza rasmi zoezi hili wiki hii ili na wengine ambao awakupata nafasi ya kuchangia damu waweze kuhamasika," amesema.

Kwa upande wake Meneja wa Kituo cha Damu Salama Kanda ya Ziwa, Dk.Iragi Ngerageza, amesema kituo hicho kina hudumia mikoa sita pia hupatikanaji wa mazao ya damu ambayo yanahitajika sana  kwa wamama wanaojifungua,hadi sasa ni kituo hicho ambacho kina  uwezo wa kuchakata damu na kupata mazao yake uhitaji ni mkubwa wa kuhakikisha upatikanaji wa damu salama.

Ametoa shukrani kwa taasisi hiyo ambayo wamekuwa wakishirikiana nao kutoa zawadi kwa wachangia damu wao ambapo wamepokea tisheti 340, kanga 200 na trei 500 kwahiyo wanategemea vitatumika vyema na kuwafikia walengwa huku akiwaomba waandishi wa habari kushirikiana nao ili kuhakikisha huduma ya damu salama inafanikiwa.

"Kila mwaka tuna adhimisha siku ya wachangia damu maana yake tunapata fursa ya kuwashukuru wale waliochangia damu kwa mwaka mzima ambayo tunayafanya kwa wiki mbili kuanzia leo hadi Juni 14,pia kuhamasisha wale ambao hawakuopata nafasi basi wajitokeze kuchangia damu kwa sababu damu ni tofauti na dawa nyingine hiyo inapatikana kutoka kwa watu ambao wamejitolea kwa hiari,kuchangia damu ni suala la upendo,kujitoa,ushujaa lakini ni zawadi," amesema Ngerageza.   

Naye Ofisa Uhamasishaji Damu Salama Kituo cha Kanda ya Ziwa, Bernadino Medaa, amesema taasisi hiyo imekuwa mdau mkubwa katika Uhamasishaji wa uchangiaji damu na katika kuelekea kilele cha maadhimisho hayo wanawashukuru wachangia wao wote ikiwemo taasisi za elimu,dini, wanasiasa na Waandishi wa Habari.

" Sasa tunaanza kazi rasmi leo timu zetu zitakuwa zinazunguka katika maeneo yote ya umma kama mnavyojua taasisi za elimu zilifungwa hivyo wataendelea kujikita katika masoko,kanisani,maeneo ya wazi,msikitini,stendi za mabasi pia tutashrikiana na timu zetu za Wilaya kuzunguka, lakini makusanyo ya damu kwa sasa siyo ya kuridhisha hivyo kila mmoja akawe balozi wa kuhamasisha mwenzie pamoja na kujitokeza kuchangia damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu," amesema Medaa.

Hata hivyo Mkurugenzi wa Taasisi ya Mashujaa wa Sikoseli Tanzania (TASIWA) Pascazia Mazeze, amesema wanahusika utoaji elimu,kuelimisha na kuelewesha jamii kuhusu ugonjwa wa sikoseli ambapo katika kuzindua wiki ya maadhimisho ya uchangiaji damu wakuja kutoa elimu ya umuhimu wa damu kulinganisha na  ugonjwa huo kwani ni kundi moja wapo linalo hitaji damu sana hivyo wanahamasisha jamii iweze kuchangia damu ili kusaidia jamii nzima ya watu wenye ugonjwa wa sikoseli.

Aidha Mwenyekiti wa Taasisi ya Mashujaa wa Sikoseli Tanzania, Josepha Chokara,wanaomba wananchi wajitokeze kwa wingi kuchangia damu ili waweze kusaidia kuokoa maisha ya mashujaa wao wa sikoseli kwani wanahitaji sana damu pamoja na watu wengine.

Habari Kubwa