Wagonjwa Rungwe wahaha  vipimo X-Ray, ultra sound

13Jan 2018
Nebart Msokwa
Nipashe
Wagonjwa Rungwe wahaha  vipimo X-Ray, ultra sound

WAGONJWA wanaohitaji huduma za vipimo vya mionzi (X- Ray) na Ultra-sound wakiwamo wajawazito katika Wilaya ya Rungwe, wanalazimika kwenda kutafuta huduma hizo nje ya wilaya yao kutokana na vifaa vya vipimo hivyo kwenye Hospitali ya Wilaya Makandana kuharibika.

Hayo yalisemwa juzi na mtaalamu wa vipimo hivyo katika hospitali hiyo, Mathias Msengi, akiongeza kuwa vifaa hivyo vimeharibika kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa na kulazimika kuazima mashine ya Ultra-sound kutoka katika Hospitali ya Misheni ya Igogwe ili kukabiliana na changamoto hiyo.

Msengi alisema pamoja na kuwapo kwa mashine hiyo ya kuazima, bado wanakabiliwa na changamoto nyingine itokanayo na ukweli kuwa yenyewe haina uwezo wa kupima umri wa ujauzito na pia kutoa taarifa za ukubwa wa uvimbe inapobainika kuwa mgonjwa ana tatizo hilo.

“Kuharibika kwa vifaa hivi kumesababisha wananchi wetu kusafiri umbali mrefu kwenda kupata huduma za vipimo hivyo Kyela na Mbeya,” alisema.

Aidha, Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo, Dk. Adelina Alfred, alisema chumba maalumu kwa ajili ya watoto wanaozaliwa kabla ya muda wao, kina tatizo la kuwa na vifaa vya joto visivyokuwa vya kisasa na hivyo kusababisha baadhi ya watoto kupoteza maisha.

 “Kwa mwezi huwa tunapoteza watoto kati ya wawili hadi watatu kutokana na vifaa vyetu vya joto kutokuwa vya kisasa. Tulivyonavyo vinaweza kuleta joto la chini ya kiwango au juu kuliko mahitaji na hivyo kusababisha vifo vya watoto,” alisema Dk. Alfred.

Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Dk. Marco Mbata, alisema ili kupambana na changamoto hizo, tayari wamefanya mazungumzo na baadhi ya wadau ambao wameanza kuwaletea misaada ya vifaa, ikiwamo kifaa cha joto kwa ajili ya kusaidia watoto wanaozaliwa kabla ya wakati. Pia wameshasaidiwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson, kushughulikia tatizo la uchakavu wa vyoo  

Alisema hospitali hiyo pia inakabiliwa na changamoto ya ufinyu wa wodi ya wazazi pamoja na ufinyu wa wodi ya wagonjwa wa nje (OPD), hivyo kusababisha wakati mwingine wagonjwa kulazwa chini.

Hata hivyo, alisema pamoja na changamoto ilizonazo, bado hospitali hiyo ina kiwango bora cha huduma kulinganisha na nyinginezo nyingi nchini.