Wagonjwa wa corona wafikia 19

31Mar 2020
Na Waandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wagonjwa wa corona wafikia 19

WATANZANIA watatu zaidi wamebainika kuwa na maambukizo mapya ya COVID-19, yanayosababisha ugonjwa wa corona kati ya wagonjwa wapya watano waliothibitishwa jana.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, picha mtandao.

Idadi hiyo mpya, imefanya wagonjwa waliobainika kuwa na maambukizi ya virusi hivyo vya corona nchini kufika 19.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, alitoa taarifa hiyo jana kupitia vyombo vya habari na kusema kati ya wagonjwa hao watano, watatu wanatoka Dar es Salaam na wawili Zanzibar.

“Hivyo sasa jumla ya wagonjwa wa COVID-19 nchini ni 19 akiwamo mgonjwa mmoja aliyetolewa taarifa na Waziri wa Afya wa Zanzibar Machi 28, mwaka huu,” alisema Ummy.

Alifafanua zaidi kuwa taarifa za wagonjwa hao wapya wa jijini Dar es Salaam zinawahusu wanaume wawili na mwanamke mmoja.

Alisema watu hao walibainika kupitia vipimo vilivyofanywa na Maabara Kuu ya Taifa akiwamo mwanamume mwenye umri wa miaka 49 aliyekutana na raia wa kigeni kutoka miongoni mwa nchi zilizoathirika.

Waziri Ummy alimtaja mwingine kuwa ni mwanamke mwenye umri wa miaka 21 ambaye ni miongoni mwa watu waliokuwa wakifuatiliwa.

“Kazi ya kufuatilia watu wote wa karibu waliokutana na wagonjwa hawa inaendelea. Tunawataka wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari ili kujikinga na ugonjwa huu,” alisema Ummy.

Ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na homa ya mapafu, ulianza kubainika kuwapo nchini kuanzia Machi 17, mwaka huu, baada ya kubainika kwa mgonjwa mmoja mkoani Arusha aliyetokea nje ya nchi, ambaye kwa sasa ameshathibitishwa kupona.

Serikali imeendelea kuchukua hatua kadhaa za kudhibiti maambukizo ya ugonjwa huo, ikiwamo kuzifunga shule zote nchini kuanzia za msingi hadi kidato cha sita na vyuo vikuu na vya ufundi kwa siku 30 kuanzia Machi 17, mwaka huu.

KAMPUNI YAJITOSA

Kampuni ya Grumeti Reserves kwa kushirikiana na Grumeti Fund, imefadhili mafunzo ya kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona katika vijiji 31 wilayani Serengeti na Bunda mkoani Mara.

Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, David Mwakipesile, alisema jana mjini hapa kuwa kwa kushirikisha wataalamu wa afya kutoka halmashauri za wilaya hizo, wamevifikia vijiji hivyo kupitia makundi mbalimbali ya vijana, wanawake na wazee.

Alisema njia zilizotumika kusambaza elimu ya kinga dhidi ya ugonjwa huo unaosambazwa na virusi vya Covid-19 ni pamoja na vipeperushi na matangazo vilivyosheheni ujumbe wa njia bora za kujikinga na kuepuka maambukizo.

“Kunawa mikono mara kwa mara kwa maji yaliyotiwa dawa, kuepuka misongamano na kukwepa kushikana mikono sambamba na kukumbatiana ni masuala muhimu ambayo wataalamu kutoka ofisi za waganga wakuu wa wilaya hizo wamefundisha wananchi katika vijiji hivyo,” alisema.

Alisema kampuni hiyo inayojihusisha na utalii na uhifadhi, imetoa kipaumbele katika mapambano dhidi ya corona ili kuunga mkono juhudi za serikali kuhakikisha taifa na wananchi wake wanapata uelewa juu ya kujikinga na ugonjwa huo ambao Shirika la Afya Duniani (WHO) limeutangaza kuwa janga la dunia.

Mwakipesile alisema kwa sasa kampuni hiyo imeazimia pia kufadhili matangazo ya moja kwa moja kupitia vyombo mbalimbali vya habari yatakayobeba maudhui ya elimu ya kinga dhidi ya kusambaa maambukizo ya ugonjwa huo katika mkoa wa Mara.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu, alisema kwa sasa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo inaendesha operesheni katika maeneo ya Mugumu na vituo vya kibiashara yakiwamo maeneo ya kupokea na kuhifadhi watalii ili kuhakikisha maagizo ya hatua za tahadhari yanafuatwa.

“Tunawashukuru wadau mbalimbali ikiwamo kampuni ya Grumeti ambao wanaendelea kusambaza elimu ya uhamasishaji kwa wananchi juu ya njia bora za kujikinga na maambukizo ya virusi vya corona,” alisema Babu.

Kwa mujibu wa Babu huenda maambukizo haya yaliyokumba dunia yote yakaathiri biashara ya utalii hususan katika mbuga kuu ya Serengeti, kutokana na ukweli kwamba biashara hiyo inategemea wageni kutoka mataifa ya Ulaya na Marekani ambazo kwa sasa zimepiga marufuku na kufunga mipaka yao.

Imeandikwa na Mary Geofrey, DAR, na Ambrose Wantaigwa, SERENGETI

Habari Kubwa