Wagonjwa wajisaidia kwenye mifuko kisa vyoo hospitali wilaya kufungwa

06Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Igunga
Nipashe
Wagonjwa wajisaidia kwenye mifuko kisa vyoo hospitali wilaya kufungwa

BAADHI ya wagonjwa wanaolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora na ndugu wanaokwenda kuwauguza, wako hatarini kupatwa na magonjwa ya kuambukiza kutokana na kujisaidia kwenye mifuko ya plastiki.

Watu hao wanatupa vinyesi hivyo kutokana na matundu ya vyoo wanayotumia kufungwa na ofisa afya baada ya kujaa.

Baadhi ya ndugu wanaowauguza ndugu zao waliolazwa katika wodi namba 3,6,8 na 9, Juma Jackson, Luciano Lazaro, Jilungano Jilelema na Amina Jeremiah, walisema  wanaposhikwa haja kubwa nyakati za usiku wamekuwa wakijisaidia kwenye mifuko ya plastiki, maarufu kama ‘Rambo’ na kisha kinyesi hicho hukitupa kwenye nyasi.

“Kwa kweli si siri, tunalazimika kujisaidia kwenye mifuko ya rambo kwani inapofika nyakati za usiku tunapata shida sana kutokana na harufu kali inayotoka kwenye vyoo kwa sababu ya kujaa, ndiyo maana wataalamu wa afya wamefikia uamuzi wa kuvifunga,” alisema Juma.

Pia waliweka wazi kwamba licha ya hospitali hiyo kukabiliwa na changamoto ya matundu ya vyoo, wanashangazwa pia kuona jirani ya majengo ya hospitali hiyo kumejengwa dampo la taka ambalo nalo limekuwa likitoa harufu kali licha ya baadhi ya viongozi wenye dhamana kupita katika eneo hilo na kuliona suala hilo kama ni la kawaida.

Kutokana na hali hiyo, wananchi hao wamemwomba Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuitembelea wilaya ya Igunga ili kujionea adha wanayoipata wagonjwa wanaofuata huduma za matibabu pamoja na ndugu wanaokwenda kuwauguza.

Mzabuni wa usafi katika hospitali hiyo, Amina Ramadhani, alisema wafanyakazi wake wamekuwa wakikumbana na changamoto kubwa ya mifuko ya plastiki ikiwa na vinyesi wanapokuwa wakifanya usafi jambo ambalo alisema ni hatari kwa usalama wa afya zao.

Kaimu Ofisa Afya wa Wilaya ya Igunga, Andrew Ndomondo, alikiri kwamba vyoo hivyo vimefungwa ili kunusuru maisha ya wagonjwa waliolazwa pamoja na watu wengine wanaofika kwa ajili ya kufuata huduma za afya.

Ndomondo alisisitiza kwamba ni muda mrefu sasa tangu alipoiandikia mamlaka inayohusika barua ili kushughulikia matengenezo ya miundombinu ya kupitisha maji taka, lakini hadi sasa hakuna utekelezaji uliofanyika.

Alionya kuwa endapo hatua za haraka hazitachukuliwa kutengeneza miundombinu hiyo, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea mlipuko wa magonjwa kutokana na vinyesi vinavyowekwa kwenye mifuko ya rambo na kutupwa ovyo kwenye manyasi yaliyopo ndani ya hospitali hiyo.

Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga, Dk. Merchades Magongo, alisema zaidi ya Sh. milioni 3.5 zinahitajika kukamilisha matengenezo ya miundombinu ya majitaka kutokana na iliyopo kuwa chakavu. Alisema ni muda mrefu tangu ilipojengwa na kuahidi kuwa tayari wameshajipanga kutengeneza  yote upya katika muda si mrefu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Igunga, Joseph Elias, alikiri kwamba jirani la majengo ya hospitali hiyo kuna dampo la uchafu na kwamba limekuwa kero kwa wagonjwa na wananchi wanaokwenda katika hospitali hiyo kutibiwa.

Hata hivyo, alisema wamejipanga kulihamisha dampo hilo huku akiwatahadharisha wananchi kutoendelea kutupa taka katika eneo hilo.

Habari Kubwa