Wahandisi watatu Ilala washushwa vyeo vyao

21Apr 2016
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Wahandisi watatu Ilala washushwa vyeo vyao

BARAZA la Madiwani na Kamati ya Fedha Manispaa ya Ilala, limewatumbua majipu wahandisi watatu waliokuwa wakisimamia ujenzi wa barabara ndani ya halmashauri hiyo kwa kuwashusha vyeo kutokana na usimamizi mbovu uliosababisha miundombinu kadhaa kujengwa chini ya kiwango.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilala, Mhe. Charles Kuyeko akifungua kikao cha Baraza la Madiwani.

Wahandisi hao ni Mkuu wa Kitengo cha Ujenzi, Japhary Bwigane na wasaidizi wake, Siyajali Mahili na Daniel Kirigiti.

Meya wa Manispaa ya Ilala, Charles Kuyeko, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana alisema barabara ndani ya halmashauri hiyo, zimekuwa zikitengewa kati Sh. bilioni moja hadi bilioni tatu, lakini wahandisi hao wamefanya usimamizi mbovu unaosababisha kujengwa chini ya kiwango.

Alitaja baadhi ya barabara zilizojengwa chini ya kiwango kuwa ni ile ya St. Mary’s eneo la Ubayaubaya, Mombasa kuelekea Moshi Bar na ya Mpiji Majohe.

Alisema barabara nyingine zimewekwa vifusi na kukaa muda mrefu bila kusambazwa.

Aliwakumbusha wasimamizi wa miradi kuwa maendeleo hayaletwi na fedha, bali usimamizi wa kuridhisha.

“Baraza lilipokaa, limegundua wasimamizi wetu wanaofanya kazi na wasimamizi wa barabara kitengo cha ujenzi, usimamizi wao ulikuwa mbovu na madiwani wamejiridhisha uwezo wa wahandisi hawa ni mdogo,” alisema.

Aliongeza: “Watu hawa wamekuwa wakiitwa mara kwa mara na kuelezwa kero zilizokuwa zikitokana na njia hizo, lakini hawakujirekebisha, wameshushwa vyeo na nafasi zao ndani ya wiki hii watateuliwa wengine,” alisema.

Alisisitiza kuwa hiyo iwe mfano kwa wengine ambao wamepewa ridhaa ya kusimamia miradi ya maendeleo waitekeleze kama ilivyokusudiwa.

“Lazima wajizatiti kwa sababu serikali ya sasa ni ‘Hapa ni Kazi tu”, hii ni `alarm' imelia tutaangalia idara moja hadi nyingine kama miradi inasimamiwa ilivyotakiwa,” alisema.

Hata hivyo, alisema barabara ambazo zimejengwa chini ya kiwango zinarudiwa upya kwa gharama ya mkandarasi, hivyo Manispaa haijapata hasara ya kifedha.

Aidha, alisema Baraza la Madiwani na Kamati ya Fedha, wamepitisha bajeti ya Sh. bilioni 85 ambayo itaboresha barabara, vituo vya afya, kujenga madarasa, kuchimba visima na maji na kero nyingine zitashughulikiwa kwa kiwango kikubwa.

Alisema wameweka kiwango hicho kwa sababu wanaamini kuwa halmashauri hiyo kupitia vyanzo vyake vya mapato vinaweza kukusanya zaidi ya hizo na kufikia Sh. bilioni 100 wakati awali ilikuwa ikikusanya kati ya Sh. bilioni 32 au Sh. bilioni 52.

Kuhusu wamachinga kuzagaa katikati ya Jiji na kuleta usumbufu kwa wengine, Meya huyo alisema wamejipanga hadi Julai, mwaka huu watu hao watakuwa wameondolewa na kupelekwa maeneo rasmi watakayotenga kwa biashara.

“Kwa sasa wamachinga wanaleta kero kwenye masoko na vituo vya daladala wamesababisha msongamano usio wa lazima. Tunajua wamejiajiri, lakini lazima kuwapo utaratibu wa kutafuta riziki,” alisema.

Alisema wanatarajia kujenga kituo cha kisasa cha daladala eneo la kiwanda cha Kiltex na Kinyerezi ambapo maeneo rasmi ya wamachinga yatatengwa.

Pia alisema manispaa hiyo inatarajia kujenga masoko kadhaa ambayo wanaamini ndiyo yatatatua kero ya kundi hilo.

Habari Kubwa