Wahitimu kidato cha 6 wapewa neno mitandao ya kijamii

25Apr 2021
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Wahitimu kidato cha 6 wapewa neno mitandao ya kijamii

WANAFUNZI wanaohitimu kidato cha sita nchini, wametakiwa kujiepusha na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na badala yake watumie elimu waliyopata ili kutafuta utatuzi wa changamoto zilizopo katika jamii.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Elirehema Doriye.

Wito huo umetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Elirehema Doriye, katika hafla ya mahafali ya 27 ya Shule ya Sekondari ya Jitegemee.

Amesema ni muhimu kwa wahitimu hao kujiandaa kuwa raia na vijana wema mtaani ili waweze kuvuna matunda bora waliyoyapata wakiwa shuleni hapo.

Amewataka wahitimu hao kubadili maarifa yao kuwa ujuzi utakaowapa fursa za kutumia rasilimali mbalimbali zinazowazunguka katika  kuzalisha mali na kukuza biashara.

“Taifa letu linatarajia mengi kutoka kwenu, kwa wale watakaoshindwa kuendelea na masomo moja kwa moja jishughulisheni na shughuli rasmi za kujiingizia kipato halali, msibweteke na kuamini kuwa ajira ni zile za kuwa ofisini. Taifa linahitaji kila mtanzania achape kazi popote alipo,” amesema Doriye.

Aidha, aliupongeza uongozi wa shule hiyo hususani walimu kwa juhudi mbalimbali wanazozifanya kutoa elimu bora kwa wanafunzi shuleni hapo na kusisitiza kuwa pamoja na suala la elimu ni wito, kada ya ualimu ni kiungo muhimu katika uhai wa Taifa.

Amesema  kama kweli taifa linataka kupata mafanikio ya kweli lazima kuwekeza kwenye walimu.

Katika mafahali hayo NIC iliahidi kutoa Sh. milioni 26 kwa ajili ya ukarabati wa mabweni na miundombinu mingine ya shule hiyo.

Kwa upande wake mkuu wa shule hiyo, Kanali Robert Kessy, mbali na kutoa pongezi kwa wahitimu, amewataka kutambua kuwa kuhitimu kidato cha sita siyo mwisho wa maisha yao ya kielimu na kujitafutia maarifa mengine.

Amewataka waelekeze akili na mitazamo yao katika kutafuta fursa mbalimbali ambazo zitawasaidia kujikwamua kimtamzamo na maisha kwa ujumla wake.

Katika Mahafali hayo jumla ya wanafunzi  289 wakiwamo wasichana 87 na wavulana 202 wamehitimu elimu hiyo ya kidato cha sita shuleni hapo.

Habari Kubwa