Wahitimu Sunshine watia fora masomo ya sayansi

26Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
KIBAHA
Nipashe Jumapili
Wahitimu Sunshine watia fora masomo ya sayansi

WAHITIMU wa kidato cha nne wa shule ya Sunshine ya Kibaha Mkoa wa Pwani wametia fora kwa namna walivyoweza kuelezea masomo ya baiolojia na uhandisi wa umeme kana kwamba ni wakufunzi waliokwisha kuhitimu  kwenye masomo hayo.

Wahitimu wa kidato cha nne wa shule ya sekondari ya Sunshine ya Kibaha Mkoa wa Pwani wakiserebuka na mwalimu wao mkuu, Francis Raphael wakati wa mahafali ya kidato cha nne jana Jumamosi shuleni hapo.

Hayo yalitokea kwenye mahafali ya 14 ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo mkoa wa Pwani na kuhudhuriwa na wazazi na walezi wa wanafunzi hao.

Rogers Titus na wenzake waliweza kuwashangaza wageni kwenye mahafali hayo kwa namna walivyomudu kuelezea moyo wa binadamu unavyofanyakazi na kisha kuufanyia upasuaji.

Hali hiyo iliibua shangwe kwa wageni waalikwa kutokana na namna Rogers na wenzale walivyokuwa wakimudu kujielezea kwa ufasaha kwa kutumia lugha ya kingereza kuhusu moyo unavyofanya kazi na kisha kuupasua.

Wanafunzi wengine walionyesha umahiri kwenye masuala ya umeme baada ya kuonyesha namna wanavyoweza kutengeneza umeme kwa kutumia vifaa mbalimbali walivyobuni wenyewe.

Mhitimu wa kidato cha nne wa shule ya Sunshine ya Kibaha Mkoa wa Pwani, Titus Rogers akionyesha umahiri wa kuelezea moyo wa binadamu unavyofanyakazi wakati wa mahalai ya 14 ya shule hiyo yaliyofanyika jana Jumamosi mkoani humo.

Wakati huo huo, Wanafunzi wanaosoma  shule za St Anne Marie Academy  ikiwemo Sunshine ya Kibaha watakaofiwa na wazazi wao na kushindwa kulipa ada ya hawatafukuzwa shule na badala yake wataendelea na masomo kama kawaida.

Ahadi hiyo ilitolewa  mwishoni mwa wiki na Mkurugenzi wa shule ya Sunshine Jasson Rweikiza kwenye mahafali ya 14 ya shule hiyo yaliyofanyika shuleni hapo Kibaha Mkoa wa Pwani.

Alisema kwa mwaka huu pekee wazazi 93 wamefariki dunia kwasababu mbalimbali na kusababisha baadhi ya wanafunzi kuacha masomo kwa kukosa ada.

Mkurugenzi wa shule za St Anne Marie Academy zinazomiliki shule hiyo ya Sunshine ya Kibaha akilishwa keki na mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo kwenye mahafali yaliyofanyika jana Jumamosi shuleni hapo.

" Tumekuwa tukipoteza wazazi wengi na mwezi huu pekee tumepoteza wazazi watatu na hali hii imekuwa ikiathiri sana wanafunzi lakini kuanzia sasa hakuna atakayefiwa ambaye atafukuzwa shule kwa kukosa ada," alisema

" Kama yuko darasa la kwanza ataendelea kusoma mpaka darasa la saba na kama ni sekondari ataendelea mpaka kidato cha nne," alisema Dk. Rweikiza ambaye  ni Mbunge wa Bukoba Vijijini CCM

Dk. Rweikiza alisema katika mpango wa kuinua taaluma shuleni hapo wameaandaa zawadi mbalimbali zikiwemo fedha taslimu kwa awatakaofanya vizuri kwenye masomo yao.

Alisema mwanafunzi atakayepata daraja la kwanza atapata sh 600,000 na atakayepata daraja la II atapata Sh 200,000 na kwamba lengo ni kuhakikisha hakuna daraja la nne wala daraja la tatu shuleni hapo.

Mkuu wa shule ya Sunshine, Frank Raphael alisema wahitimu hao wameandaliwa vizuri kitaaluma na wanatarajiwa kufanya vizuri kwenye mitihani yao.

Mkurugenzi wa shule za St Anne Marie Academy zinazomiliki shule hiyo ya Sunshine ya Kibaha akilishwa keki na mmoja wa wanafunzi wa shule hiyo kwenye mahafali yaliyofanyika Jumamosi shuleni hapo.

Alisema wanafunzi hao wamewezeshwa kufikia hapo na walimu wenye taaluma na uzoefu wa kutosha huku akimshukuru Mkurugenzi wa shule hizo, Dk. Rweikiza kwa kuendelea kufanya maboresho.

Alisema Dk. Rweikiza amewawezesha kupata maabara iliyosheheni vifaa vya kutosha, vifaa vya kufundishia kama vitabu, projekta, mashine ya kudurufia, maji safi, ulinzi na huduma bora za afya.

Habari Kubwa