Wahudumu wa wakimbizi wakutana kujadili maboresho ya huduma hiyo

28Nov 2021
Neema Emmanuel
Mwanza
Nipashe Jumapili
Wahudumu wa wakimbizi wakutana kujadili maboresho ya huduma hiyo

​​​​​​​VIONGOZI mbalimbali wanaohusika kutoa huduma kwa wakimbizi nchini wamekutana kwa siku tatu ili kuboresha huduma kwa kundi hilo na kuhakikisha serikali inayolitunza inafanya kwa kuzingatia maslahi mapana ya Taifa.

Akizungumza na waandishi wa habari Kamishina wa Polisi na Mkurugenzi Msaidizi wa Makambi na Makazi ya Wakimbizi Nsato Marijani, amesema wamekutana ili kuweka vichwa vyao pamoja na kupeana taarifa jinsi wanavyoendelea na shughuli ya kuhudumia wakimbizi kati ya serikali ambayo kimsingi ndio mwenyeji wa wakimbizi na waomba hifadhi wote waliopo nchini.

Amesema katika shughuli hizo za kuhudumia wakimbizi ni muhimu wakakaa pamoja na kuangalia nini kimefanyika na katika hicho walichofanya mafanikio ni kiasi gani, changamoto ni zipi na wanapaswa kufanya nini ili kumaliza changamoto hizo.

"Kama mnvyofahamu jukumu la kuhudumia wakimbizi linapaswa kufanywa na jumuiya zote za kimataifa, hivyo UNHCR na mashirika mengine ya Umoja Wa Mataifa yanaisaidia serikali ya Tanzania kuhudumia wakimbizi," amesema marijani .

Ameongeza kuwa hakuna sehemu serikali haitoi huduma kwa wakimbizi, kila idara na wizara ya serikali kwa njia moja ama nyingine inafanya shughuli za wakimbizi, wapo wachache ambao wapo karibu sana sasa hao tumefanikiwa kuwaita kama watu wa Mahakama, Polisi Magereza, Uhamiaji, huduma ya watoto, adhabu mbadala pamoja na idara inayohusika na shughuli za wakimbizi.

Habari Kubwa