Wahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya mtoto

24Sep 2021
Pendo Thomas
KIGOMA
Nipashe
Wahukumiwa kunyongwa hadi kufa kwa mauaji ya mtoto

WATU wawili wakazi wa kijiji cha Gwanumpu, Kakonko mkoani Kigoma, wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya mauaji ya mtoto wa miaka 12 waliyemteka wakidai wapewe Sh. milioni tano na baadaye kuuzika mwili wake ukiwa umekalishwa na kufungwa kichwani, usoni na miguuni.

Watuhumiwa wa mauaji.

Waliohukumiwa kwenye kesi hiyo ya mauaji ya kukusudia namba 18/2021 katika Mahakama Kuu kanda ya kigoma ni Tabibu Nyundo na Thobias Mtakiyicha. Walidaiwa kutenda kosa hilo Januari 27, 2019 baada ya kumteka mtoto na kutuma ujumbe mbalimbali wa simu kwa jirani wa wazazi wa mtoto.

Sehemu ya ujumbe ulisomeka” ‘’Tumemkamata mtoto wa Buchumi tunataka Sh. milioni tano mwambie baba yake atume pesa hizo ili tumwachie.’’

Upande wa Jamuhuri ukiongonzwa na mawakili Happiness Mayunga na Antia Julius, uliwakilishwa na mashahidi tisa wakiwamo baba mzazi, jirani aliyetumiwa ujumbe wa simu, ofisa mtendaji, mwenyekiti wa kijiji, askari polisi na daktari.

Ilielezwa wakiwa kwenye harakati za kumtafuta mtoto bila mafanikio, Januari 30, 2019 walilazimika kuchangisha fedha kwa wanakijiji na kupatikana Sh. 700,000  na mzazi wa mtoto kuongezea Sh. 800, 000 hivyo kufikia Sh. Milioni 1.5 ambazo walizituma kwa namba iliyotuma ujumbe huo baada ya kukubaliana kushusha kiwango kutoka Sh. milioni tano.

Ilipofika Februari 2, 2019 walikwenda ofisi za watoa huduma wa simu kuifuatilia namba waliyoitumia pesa na kubainika fedha hizo zilitumwa kwenda kwa Thobias Mtakiyicha ambaye wanamfahamu na kuanza jitihada za kumtafuta nyumbani kwake.

Walidai kuwa baada ya kufika kwake hawakumkuta na kupewa maelekezo kuwa amekwenda shambani yeye na rafiki yake, hivyo kuchukua hatua za kumfuatilia lakini walimpata rafiki yake na alionekana mwenye wasiwasi na alipo ulizwa juu ya mwenzake, alisema yuko njiani akirejea nyumbani na laini ile iliyotumiwa fedha anayo.

Hatua hiyo, walidai kuwa ilisaidia kupatikana fedha hizo ambazo zilitolewa kwenye simu kisha kutumika kama kielelezo cha shauri hilo.

Wakiwa rumande Februari 6, mwaka huo,  shahidi wa tisa wa Jamuhuri alidai kuwa aliitwa na mmoja wa washtakiwa hao na aliposogea walimwambia tunaomba waseme ukweli ndipo wakaweka wazi kuwa walimteka mtoto kisha kumuua na kumzika na kwamba wako tayari kwenda kuonyesha eneo hilo.

Ilidaiwa kuwa polisi waliwachukua hadi eneo alipozikwa mtoto kisha kuwarudisha washtakiwa na baadaye kwenda na wanakijiji pamoja na familia ya mtoto kufukua kaburi hilo ambalo walikuta mwili ukiwa umezikwa.

Washtakiwa wakitetewa na mawakili wawili Sylvester Sogomba na Elizabeth Twakazi, walikana mashtaka hayo na kudai ni ya uongo na utetezi wao kwa uchache walidai wameunganishwa kwenye kesi wakati hawafahamiani.

Pia walidai maelezo yaliyowasilishwa na polisi si ya kweli waliyatoa baada ya mateso makali waliyopewa na kuwa mmoja ya mshtakiwa alikuwa na mgogoro na baba wa mtoto, hivyo kuna uwezekano ametumia mwanya huo kumsingizia.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Lameck Mlacha, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, alisema washtakiwa wameidanganya mahakama kuwa hawafahamiani wakati ni vijana wanaoishi kijiji kimoja.

Kuhusu madai kuwa walipigwa na polisi pasipo kutoa vielelezo vyovyote vya kiafya pia maelezo waliyompatia askari polisi yalijawa hatia na kujuta na yalifanikisha kupatikana kwa mwili wa mtoto pamoja na laini ya simu iliyotumiwa fedha kukutwa nayo.

‘’Adhabu ni moja tu kunyongwa hadi kufa. Hii  adhabu siipendi lakini mikono yangu imefungwa. Nafasi ya rufani iko wazi,” alisema Jaji Mlacha.