Waiomba serikali isaidie kulipwa fidia

13Aug 2020
Samson Chacha
Tarime
Nipashe
Waiomba serikali isaidie kulipwa fidia

WAKAZI zaidi ya 200 wa kitongoji cha Nyamichele, Kijiji cha Nyakunguru, wilayani hapa, wameiomba serikali iwasaidie kulipwa fidia za mali zao yakiwamo mashamba.

mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mtemi Msafiri, picha mtandao

Walidai kuwa Mgodi wa Barrick North Mara unaozunguka maeneo yao, ulifanya tathmini tangu mwaka 2013 hadi sasa bila mafanikio ya kulipwa fidia.

Wakitoa kilio katika mkutano wa kitongoji cha Nyamichele na Kijiji cha Nyakunguru, kata ya Kibasuka, chini ya Mwenyekiti wa kijiji hicho, Chacha Sasi, aliyekuwa diwani kata hiyo, Joyce Manyata, walisema kuwa wananchi wao waliofanyiwa tathmini na mgodi huo kwa ajili ya kulipwa fidia tangu mwaka 2013 hadi sasa, hawajalipwa.

Walidai maeneo yao waliokuwa wakilima mazao ya chakula, wengi walisitisha kufanya shughuli za kilimo na wenye nyumba zilizokumbwa na zoezi hilo la tathimini, nyumba zao zimebomoka kutokana na kutofanyiwa ukarabati.

"Wananchi wa Nyamichele na Nyakunguru tunaiomba serikali ya awamu ya tano ya kuwatetea wanyonge chini ya Rais John Magufuli kuhimiza Mgodi wa Barrick North Mara ili uweze kuwalipa fidia wananchi waliofanyiwa tathimini.”

Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mtemi Msafiri, alisema maeneo ya kitongoji cha Nyamichele, kijiji cha Nyakungu, wananchi walifanyiwa tathmini ili walipwe fidia kama maeneo mengine ambayo kwa sasa ulipaji unaendelea vijiji vinavyozunguka mgodi huo yakiwamo maeneo ya Matongo na Nyabichune.

Alisema tatizo lililopo katika maeneo yaliyofanyiwa tathmini, baadhi ya wananchi wamepanda mazao usiku na kutegesha miche ya kahawa, migomba, katani na miti ya matunda katika eneo moja kwa nia ya kuhesabiwa miche hiyo ili ilipwe, kitendo ambacho kinakwamisha zoezi hilo kwa wananchi kukosa uaminifu.

Kadhalika, Msafiri alisema baadhi wamekuwa mawakala kwa kununua maeneo ya watu wengine kwa kutegesha wakati awali tathimini ikifanywa hawakuwapo.

“Tunaendelea kufanya uhakiki wa majina ya watu wanaostahili kulipwa fidia na kuondoa majina ya watu wasio na sifa waliojipenyeza kwa nia ya ovu ya kutaka kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu,” alisema.

Aliwataka wananchi hao kuwa na subira kwa kuwa ulipaji fidia unaendelea hatua kwa hatua na sawa ulipaji huo uko katika vijiji vya Matongo na Nyabichune na baadaye kuendelea katika maeneo mengine.

Habari Kubwa