Waishukuru serikali kwa kuwakumbuka

11Jan 2020
Said Hamdani
Masasi
Nipashe
Waishukuru serikali kwa kuwakumbuka

UONGOZI wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi Masasi mkoani Mtwara (FDC), umeishukuru serikali kwa kuwapatia fedha Sh. milioni 570.1 kwa ajili ya ukarabati wa majengo ya chuo na kujenga majengo mengine mapya sita.

Umesema chuo kilikuwa kinakabiliwa na tatizo la uchakavu wa majengo yake hasa mabweni ya wanafunzi na madarasa, hali iliyousukuma uongozi kuiomba fedha serikalini.

Mkuu wa chuo hicho, Alfani Mshana, alitoa shukrani hizo kwa serikali jana alipozungumza na Nipashe ofisini kwake kuhusu vikwazo vinavyokikabili chuo hicho.

Mshana alisema tayari wameshapokea fedha hizo zilizotolewa na serikali kwa ajili ya ukarabati wa majengo yote chakavu.

Alisema ukarabati wa majengo na ujenzi wa majengo mapya sita katika chuo hicho tayari umeshaanza na baadhi ya majengo ukarabati wake unatarajia kukamalika hivi karibuni.

"Tunamshukuru sana Rais John Magufuli kwa kutupatia fedha hizi Sh. milioni 570.1 ili tukarabati majengo ya chuo hiki na kujenga mengine mapya, likiwamo bweni la wanafunzi," alisifu.

Alibainisha kuwa chuo hicho kina wanafunzi wapatao 300 ambao ni wasichana na wavulana, hivyo uboreshaji huo unaofanywa na serikali, utasaidia kukipa hadhi.

Hata hivyo, Mchana aliweka wazi kuwa bado jamii hasa ya mikoa ya kusini haijawa na mwamko chanya wa kutambua thamani ya uwapo wa chuo hicho, akieleza kuwa hata hamasa ya kuwapeleka watoto wao kusoma hapo bado ni ndogo.

Alisema chuo hicho kinatoa elimu ya fani mbalimbali kwa wanafunzi, ikiwamo stadi za maisha, ushonaji, uashi, mapishi, utengenezaji wa magari na umeme wa majumbani na magari.

Mshana alisema kupitia fani hizo zinazotolewa chuoni hapo, tayari chuo hicho kimeshazalisha wanafunzi wengi nchini ambao kwa sasa wamejiajiri na baadhi wameajiriwa katika sekta za umma na binafsi.

"Licha ya serikali kutupatia fedha hizi kwa ajili ya vikwazo vilivyokuwapo vya uchakavu wa majengo, tatizo lingine ni upungufu wa walimu, tuna walimu saba wakati mahitaji ni zaidi ya hapo," alibainisha.

Mwalimu Maliki Liyanga wa chuo hicho, pia aliishukuru serikali kwa kutoa fedha za ukarabati na ujenzi wa majengo mapya chuoni hapo.

Habari Kubwa