Waislamu wajitosa dawa za kulevya

20Feb 2017
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Waislamu wajitosa dawa za kulevya

JUMUIYA ya Taasisi za Kiislamu Tanzania, imeitaka serikali kuendeleza vita ya dawa za kulevya kwa kuwahusisha pia watumiaji na wanaohusishwa wakiwamo wapiga debe na mateja wote wa mitaani.

Msemaji wa taasisi hiyo, Sheikh Rajab Katumba.

Hayo yalielezwa jijini Dar es Salaam jana na Kaimu Msemaji wa taasisi hiyo, Sheikh Rajab Katumba, wakati akizungumza na waandishi wa habari juu ya msimamo wao katika operesheni ya dawa za kulevya inayoendelea nchini.

Sheikh Katumba alisema kama serikali ina wajibu wa kuhakikisha wote wanaohusika na utumiaji wa dawa hizo wanachukuliwa hatua bila kuwaonea haya wengine.

Hata hivyo, alisema utaratibu unaotumika wa wakuu wa mikoa kutaja majina ya watumiaji au wanaohusishwa na dawa za kulevya, si sahihi na kwamba kufanya hivyo ni kudhoofisha nguvu na kuufanya uingiliwe na wanasiasa.

"Watanzania hasa sisi Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu, tunataka vita hii iwe ya dhati na kusiwe na malengo ya pembeni ikiwa kama watumiaji wote wanaotumia au kuhusishwa wakiwamo wasanii na wapiga debe ambao ni wateja, hawajasombwa na kisha kupimwa damu na kushtakiwa, itakuwa ni haki ya mwananchi kuamini kuwa hii ina malengo tofauti," alisema na kuongeza:

"Pamoja na nia ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, kuongoza na kuendesha vita hii, tunaomba vyombo vyenye weledi ndiyo viwe viongozi wa operesheni badala ya wanasiasa ambao kwa kiasi kikubwa siyo wenye weledi na fani hii."

Sheikh Katumba alisisitiza kuwa taasisi hiyo inaunga mkono juhudi za serikali kwa kuwa hawapendezwi kuona nguvu kazi ya vijana ikiendelea kuteketea kwa kutumia dawa za kulevya.

"Tunapongeza hatua ya kupambana na mafisadi na watumiaji wa dawa za kulevya nchini. Lakini hatari ya vita hii kuwa nje ya vyombo vya dola vyenye mamlaka ya kisheria, kutasababisha kushuhudia kutolewa matamko ya kuropoka yaliyo nje ya Katiba na sheria," alisema Sheikh Katumba.

Mbali na hilo, aliiomba Tume ya Maadili kuhakiki mali za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Makonda kama ilivyopendekezwa na wabunge ili kuondoa shaka katika umiliki wake.

Alisema misaada ambayo Makonda anasaidia baadhi ya taasisi, amekuwa akidai anaipata kwa marafiki.

Habari Kubwa