Waitaka NEC kufunga CCTV vituo vya kura

19Jun 2019
Enock Charles
Dar es Salaam
Nipashe
Waitaka NEC kufunga CCTV vituo vya kura

WADAU wa uchaguzi wameishauri Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufunga kamera fiche (CCTV) kwenye vituo vyote vya kupiga kura ili kuepusha malalamiko ya kuibiwa kura yanayoibuka kila unapofanyika uchaguzi nchini.

CCTV

Akizungumza katika mkutano wa tume na wawakilishi wa makundi maalum ya vijana, walemavu na wanawake uliofanyika Dar es Salaam jana, mwakilishi wa Kongamano la Msaada wa Kisheria kwa Vijana, Ramadhani Juma, aliishauri tume kutumia kamera fiche ili kudhibiti wizi wa kura wakati wa uchaguzi.

“Pamekuwa na malalamiko sana ya kura kuibiwa, je, tume haioni umuhimu wa kuweka CCTV Camera kwenye hizi 'polling stations' (vituo vya kupiga kura), ili kuweka ulinzi wa kura na kuondoa malalamiko?" Ramadhani alihoji.

Akijibu hoja hiyo, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage, alisema sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa katika kusimamia uchaguzi nchini, zikitumiwa vizuri zinajitosheleza kwa ulinzi wa kura.

“Sheria zetu, kanuni zetu na taratibu zetu kama zitazingatiwa, uchaguzi wetu ni shirikishi na hakutakuwa na sura hiyo ambayo inaonekana.

"Tatizo ni kwamba tunaacha hivi vyombo vyenyewe, tunatafuta namna zingine zisizofaa, Jaji Kaijage alisema.

Katika mkutano huo, mwakilishi wa Taasisi ya Elimika Tanzania, aliyejitambulisha kwa jina la Masawiri, alihoji msimamo wa NEC kuhusu wananchi kukaa ama kutokaa umbali wa mita 200 kutoka kwenye vituo vya kupiga kura baada ya kuwa wamepiga kura.

Hoja hiyo ni moja ya mapendekezo ya vyama vya upinzani vikiamini kwa kufanya hivyo, kutakuwa na ulinzi imara wa kura.

Akijibu hoja hiyo, Jaji Kaijage alisema: “Baada ya Uchaguzi Mkuu 2015, mtakumbuka palikuwa na kesi ya Kibatala iliyofunguliwa kuhusu masuala hayo na uamuzi ulitolewa ni kwamba mara baada ya watu kupiga kura, wanarudi nyumbani. Huo ndiyo uamuzi wa mahakama na ndiyo sheria. Sasa hivi, hakuna cha mita 100, 200 wala 300."

Mkutano huo ni sehemu ya mikakati ya NEC kukutana na wadau mbalimbali wakati ikijipanga kwa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura unaotarajiwa kufanyika mwezi ujao.

Habari Kubwa