Waitara kupambana na wakandarasi wababaishaji

25Apr 2021
Gwamaka Alipipi
Dodoma
Nipashe Jumapili
Waitara kupambana na wakandarasi wababaishaji

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, amesema atapambana na wakandarasi wababaishaji wanaoidanganya Serikali kuwa wana vigezo, lakini wanajenga barabara zilizo chini ya viwango na kusababisha gharama kubwa za matengenezo ya mara kwa mara.

NAIBU Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara.

Mbali na hilo, amesema atashughulika na wafanyakazi wanaoshirikina na wakandarasi kuihujumu miundombinu ya barabara, madaraja, reli, bandari, vivuko na viwanja vya ndege.

Ameyasema hayo katika kikao kazi kilichojuisha menejimenti na wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, pamoja na mambo mengineyo alipokea taarifa ya bodi hiyo.

Aidha, Waitara amwupongeza Mfuko wa Barabara Nchini kwa namna wanavyosimamia matengenezo ya barabara kwa uharaka unaoendelea kufanywa na Wakala wa Barabara Nchini  (TANROADS), pamoja na Wakala wa Barabara za vijijini na mijini (TARURA).

"Tutahakikisha tunapunguzana humu humu ndani na ukigundua kuwa wewe siyo mwenzetu ujitafakari kuwa wa moto au baridi na siyo kuwa vuguvugu, tunahitaji watumishi wazalendo na wakandarasi wenye sifa na weledi", amesema Waitara.

Mbali na kueleza hayo, Waitara amewataka watendaji kuongeza kasi katika maamuzi hasa pale inapotokea dharura ya madaraja na barabara kukatika na kusababisha wananchi kukosa huduma mbalimbali za kijamii.

Naye Meneja wa Mfuko wa Barabara, Eliud Nyauhenga, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bodi hiyo, amesema mfuko umeweza kufadhili tafiti mbalimbali zinazofanywa kwenye ujenzi wa gharama nafuu, ili kujenga barabara nyingi na imara.

Nyauhenga amesema kuwa Bodi ya Mfuko wa Barabara Nchini pia imeendelea kutoa elimu kwenye ngazi zote kuhusu  matumizi bora ya barabara, ili kuilinda miundombinu hiyo na kupunguza gharama kubwa za matengenezo.

Habari Kubwa