Waitara: maRC, DC hawana mamlaka kusimamia uchaguzi

05Sep 2019
Augusta Njoji
Dar es Salaam
Nipashe
Waitara: maRC, DC hawana mamlaka kusimamia uchaguzi

BUNGE limeelezwa kuwa Kanuni na miongozo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa za Mwaka 2019 hazijampa mamlaka yeyote awe Mkuu wa Mkoa au Mkuu wa Wilaya kuwa msimamizi wa uchaguzi.

Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mwita Waitara.

Aidha, wabunge wa upinzani wameondolewa hofu kuwa uchaguzi huo utakuwa huru na haki hivyo hawana sababu ya kuhofia.

Hayo yameelezwa leo na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mwita Waitara alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Kibamba(Chadema) John Mnyika.

Katika swali lake, Mnyika amehoji ni kwanini wakuu wa mikoa na wilaya wamepewa mamlaka kwenye usimamizi wa uchaguzi wakati ni makada wa Chama cha Mapinduzi(CCM) na kuonesha hofu kuwa uchaguzi huo hautakuwa huru na haki.

Akijibu swali hilo, Waitara amesema uchaguzi huo unasimamiwa na waziri mwenye dhamana.

Aidha amesema kanuni hizo zimezingatia miongozo huku akidai kuwa si kila wanapoitwa kutoa maoni sio lazima kichukuliwe kila kitu bali watalaam hukaa na kuangalia Katiba, sheria na miongozo mbalimbali halafu inaamuliwa.

"Kanuni hizi hazijampa dhamana  yeyote mkuu wa wilaya au mkoa kusimamia uchaguzi.Nikuombe usiwe na hofu Mnyika uchaguzi huu utafanyika huru na haki tujipange tukutane kazini,"amesema.

Habari Kubwa