Wajasiliamali watakiwa kutembelea mabanda ya huduma za urasimishaji

05Dec 2021
Neema Emmanuel
Mwanza
Nipashe Jumapili
Wajasiliamali watakiwa kutembelea mabanda ya huduma za urasimishaji

WAJASILIAMALI wa Afrika Mashariki wametakiwa kutembelea mabanda ya taasisi zinazojishughulisha na utoaji huduma za kuwezesha urasimishaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi nchini ili kupata elimu itakayoweza kuwasaidia kukua kwa pamoja.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,Bunge,Kazi,Vijana,Ajira Walemavu) Jenista Mhagama, wakati akizungumza kwenye siku ya Tanzania katika maonesho ya 21 ya wajasiriamali wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ya Jua Kali, Nguvu Kazi yanayofanyika katika uwanja wa Rock City Mall mkoani Mwanza huku Tanzania ikiwa ni wenyeji wa maonesho hayo.

Amesema serikali zote katika Jumuiya ya Afrika Mashariki zinaendelea kutekeleza adhima ya kurasimisha biashara kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiriamali huku uboreshaji wa mazingira ya biashara, bidhaa na huduma ambazo zimezalishwa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na kuzirasimisha biashara na bidhaa zao ni jambo la msingi

"Ndio maana maonesho haya sisi hapa Tanzania tumeamua kualika taasisi zile muhimu zinazoshughulika na utoaji wa huduma za kuwezesha urasimishaji wa shughuli mbalimbali za kiuchumi katika taifa letu,mmewaona hapa tunao TBS,NSSF,TMDA,TRA na taasisi nyingine nyingi, hivyo mkatembele katika mabanda yao ili mpate elimu,". Ameeleza Waziri huyo.

Anasema maonesho hayo Mhagama yanawasaidia kutengeneza mshikamano mkubwa zaidi kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki,kufahamiana,kubadilishana ujuzi wa uzalishaji bidhaa kwenye sekta ya ujasiriamali ambao kesho yake wajasiriamali ndio watatengenezeana masoko kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine.

Habari Kubwa