Wajasiriamali Kyela waeleza changamoto wanazokutana nazo

26Jan 2021
Grace Mwakalinga
MBEYA
Nipashe
Wajasiriamali Kyela waeleza changamoto wanazokutana nazo

Baadhi ya wasichana Wajasiriamali  kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Kyela na Jiji la Mbeya, wamesema miongoni mwa vikwazo vinavyosabisha washindwe kutimiza azma yao ya kujikwamua kiuchumi ni  wakopaji wa bidhaa zao kushindwa kulipa fedha kwa wakati sambamba ukosefu wa mitaji.

Waliyaeleza hayo  jana, wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyoandaliwa na  Taasisi ya Tanzania Data Lab (Dlab) ambayo yaliendeshwa kwa kushirikiana na Shirika la PEPFAR yenye lengo la kuwajengea uwezo wajasiriamali wasichana waweze kujikimu kiuchumi ili kuondokana na mambo yatakayochangia kujiingiza kwenye vishawishi vya maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.

Shukuru Mwakamala, mmoja wa wajasiriamali hao kutoka Kata ya Iganjo jijini Mbeya alisema anakabiliwa na vikwazo vingi kwenye biashara yake ya ununuzi wa mboga na matunda.

Vikwazo hiyo ni wateja wanaokopa bidhaa hiyo kushindwa kurejesha fedha kwa wakati sambamba ukosefu ya mitaji katika kuendesha biashara.

Alisema biashara yake ya matunda na mboga ambayo ananunua kutoka Wilaya ya Rungwe na maeneo mengine ya Mkoa wa Rukwa licha ya wateja kukopa na kutorejesha  fedha kwa wakati pia ukosefu wa wateja wa kutosha kununua bidhaa zake ikiwemo  maparachichi kutokana na hali ya maisha ilivyo sasa.

"Moja ya vikwazo tunavyokabiliana navyo ni mitaji, mabinti tuna nia ya kujikwamua kiuchumi lakini vikwazo ni vingi ikiwemo mitaji hali inasababisha hata bidhaa wanazoziuza kutokuwa na faida, lingine ni wateja kukopa na kushindwa kurejesha fedha," alisema Mwakamala.

Baitha Mwangosi kutoka wilayani Kyela, anajishughulisha na uuzaji wa genge na viatu vya kimasai alisema kikwazo kinachokwamisha ashindwe kufikia malengo mazingira ya kibiashara yalivyo ambayo yanachangia kukosa wateja wa kutosha.

Mratibu wa Mafunzo hayo, Somoe  Mkwachu kutoka  Taasisi ya Tanzania Data Lab (Dlab), ambao wanaendesha Program ya Data4Her alisema wamejikita kuwajengea uwezo mabinti namna ya kuendesha biashara zao kwa kutumia data.

Alisema data ina nafasi kubwa katika kuboresha biashara zao kwani zinatoa muongozo wa namna ya kuendesha na kupata faida kulingana na mazingira  yaliyopo.

Alisema jumla ya washiriki 35 ambao ni mabinti wenye umri miaka kati ya 18- 35 kutoka Halmashauri za Wilaya Kyela na Jiji la Mbeya wanapatiwa mafunzo  ya matumizi ya data kusaidia ukuaji wa biashara zao kwa muda wa siku tano jijini Mbeya.

"Tulianzisha mafunzo haya kwa lengo la kuwasaidia mabinti kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli zao za ujasiriamali wanazozifanya hata kwa wale ambao hawana biashara wanajengewa uwezo wa namna ya kuanzisha na kuendesha biashara zao kwa kutumia data, tulibaini watu wengi wanashindwa kutimiza azma zao kwa sababu ya kutokuwa na uelewa namna ya kufanikiwa kibiashara kwa kutumia mazingira wanayoyazunguka,"alisema Mkwachu.

Habari Kubwa