Wajawazito wapimwa juu ya meza, uzito wa mtoto kwenye tawi la mti

22Jan 2021
Dinna Stephano
Tarime
Nipashe
Wajawazito wapimwa juu ya meza, uzito wa mtoto kwenye tawi la mti

NYAGISYA ni kijiji kilichoko katika Kata ya Kiore wilayani Tarime mkoani Mara, ambacho hadi sasa miaka 12 ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ya Afya ya Msingi (MMAM), unaelekeza kiwe tayari kimepata zahanati, lakini kukosa kwake kunawapa makali ya maisha wakazi wake.

Kukosekana kwa huduma hiyo, moja ya waathirika wakuu ni wajawazito na watoto ambao wanalo hitaji la lazima, kuanzia kiafya, kijamii pia kisheria chini ya rungu la MMAM.

Hata hivyo, watekelezaji wa mpango huo hawana muda wa kupoteza, wamebuni mpango mbadala chini ya maelekezo ya 'kliniki inayohama', wameteua jengo la shule na miundombinu yake kuwa mahitaji ya kliniki na tayari wanatekeleza majukumu yaleyale kama ya zahanati na kituo cha afya.

Uchunguzi wa Nipashe, unabaini ni hatua mbadala kuwapunguzia wahitaji adha ya kutembea umbali wa kati Km mbili kwenye Zahanati ya Gamasara na Km nne iliko Zahanati ya Mtana, zote ziko kata jirani na hospitali ya wilaya inapatikana umbali wa Km 14. Nauli za huduma pekee ya pikipiki ni kati ya Sh. 3,000 na 5,000.

Vilevile, imegundulika kuwapo migogoro ya wanakijiji hao wanapokwenda kutibiwa katika moja ya zahanati hizo wananyima huduma.

Mpango huo mbadala unazibebesha majukumu meza na viti vya wanafunzi, kuwa sehemu ya mahitaji maalum ya kufanikisha kliniki ya mjamzito, hali kadhalika matawi ya miti iliyo jirani ni mahitaji mardhawa kufanikisha kliniki ya mtoto na vyote vimewezekana.

Kwa vipi? Hapo ndipo Nipashe ikawa shuhuda wa namna MMAM inavyotekelezwa, wakati kiti kikiendelea na wajibu wake wa siku zote, meza inakuwa kitanda maalum cha mjamzito na nje ya darasa.

Vivyo hivyo, kwa mahitaji ya mwana kliniki ambaye ni mtoto, miti iliyo nje ya mazingira ya madarasa ambayo ni mahususi kwa ajili ya maslahi ya mazingira, nayo inapewa matumizi mapya ya kuwa nyenzo sahihi ya kuning'iniza mizani hata uzito wa mtoto ukajulikana kuhitimisha mahitaji ya kliniki.

Katika ufanikishaji wa kliniki hiyo tembezi juzi, Nipashe ilishuhudia mwitikio mkubwa wa wanakijiji cha Nyagisya na huenda wengine toka jirani, kukiwa na mjumuiko mkubwa wa wajawazito na kinamama wenye watoto.

Hata hivyo, ilibainika kwamba madarasa hayo yanatumika muda wa mchana wanafunzi wakiwa wamekwenda kula, wanaohudumiwa na ratiba ya wahudumu wa kliniki watatu, japo siku ya ushuhuda wa gazeti walikuwa na udhuru alikuwapo mmoja.

Katika kuhakikisha kuwa huduma haikosekani kwa mujibu wa ratiba, wakazi hao wameandaa mbadala wa ofisi ya kijiji, ambako kuna godoro maalum walilonunua kwa kuchangishana kuwahudumia.

Ufafanuzi wa Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Nyagisya, Ghati John, kwa mwandishi wa gazeti hili ni kwamba sababu za huduma hizo kufanyika mahali hapo ni kutokana na kuwapo mgogoro kati ya kata yao ya Kiore na kata jirani ya Manga.

"Tukiwa hatuna vikao na hakuna watu wengi tunaowahudumia, tunawaachia ofisi wanawahudumia wajawazito.

"Ninawapongeza wananchi kwa kujitolea kuhakikisha tunajenga zahanati, wagonjwa na wajawazito wanateseka sana, uongozi wa kijiji tulikaa na uongozi wa shule tukashauriana eneo likapatikana la kujenga zahanati.

"Ninawaomba wadau mbalimbali waguswe watusaidie tukamilishe ujenzi," alisema.

Kwa mujibu wa MMAM, kila kijiji kinapaswa kuwa na zanahati, kata iwe na kituo cha afya, hali kadhalika hospitali inapatikana wilayani.

Vilevile, mwandishi alithibitishiwa kalenda ya kliniki inayohama kwamba, kijijini Nyagisya inapatikana mara moja kila mwezi, walengwa wakuu wakiwa ni wajawazito na watoto.

WANAOHUDUMIWA

Furaha Joseph, mkazi wa kijiji hicho, alisema: "Mimi ni mmoja wa kinamama tunaoteseka kuitafuta huduma ya afya, hatuna zahanati.

"Ukiugua au kwenda kupata huduma ya kliniki, mpaka ujipange uwe na nauli Sh. 3,000 ya pikipiki kwenda Mtana na 5,000 kwenda hospitali ya wilaya, kama hauna inabidi utembee kwa miguu, inachosha."

Happiness Johanes, mkazi mwingine wa kijiji hicho, alitaja adha nyingine ya kuhudhuria zahanati jirani ya Mtana, huwa wanakataliwa na kuelekezwa kwenda Zahanati ya Gamasara au hospitali ya wilaya, akiitaja moja ya shinikizo lililowafanya kudai kliniki tembezi kijijini kwao.

"Tukienda Mtana, wauguzi wanatuambia tunawasumbua, 'mnakuja tu kurundikana hapa', ukiwa unaanza kliniki, wanakwambia uende hospitali ya wilaya.

"Tunashukuru serikali yetu ya kijiji ilikakaa ikaona ni kwanini tuendelee kuteseka, tukaona ni bora huduma ya kliniki tuifanye hapa kwetu hata kama ni chini ya mti, inatusaidia kupunguza umbali na gharama za nauli na kauli mbalimbali za kukatisha tamaa.

"Umeshuhudia mwenyewe kwa macho yako, huwa tunapima hapa chini ya mti, mvua ikinyesha, tunahangaika sehemu ya kupimia na kujikinga.

"Ikinyesha, tunaenda ofisi ya kijiji, nako wakiwa na vikao vyao, tunaondoka tena, tunaenda shuleni, tunaomba tunapewa darasa.

"Lakini sasa hivi wanafunzi wamejaa, hakuna madarasa, inabidi tusubiri wanafunzi wakienda kupata chakula, ndiyo tunaingia, kama hakuna mvua, tunakaa chini ya mti.

"Nesi anafunga kikoi juu ya kenchi, watoto wanapimwa uzito, kwa wajawazito wanaunganisha madawati au juu ya meza, analala anapimwa kuangalia kimo cha mtoto, mlalo, mapigo, kama anacheza, huduma anapata zote isipokuwa uzito na wingi wa damu hatupimwi.

"Ofisi ikiwa wazi, kuna godoro wananchi tulinunua linawekwa chini ya sakafu, mjamzito unalala, nesi anapiga magoti chini anakupima.

"Tukiwa nje, wanaweka meza mjamzito unalala juu ya meza, unapimwa, meza tunaazima shuleni," alibainisha.

Simulizi nyingine ni kutoka kwa Rhobina Meng'anyi, alisema huduma hiyo wanayoipata chini ya mti ni huruma ya serikali ya kijiji na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime baada ya kuona wajawazito na watoto wanateseka kupata huduma.

"Mama mkwe wangu alikufa njiani akiwa anaenda kujifungua, alivuja damu nyingi kutokana na mitikiso ya pikipiki, barabara mbovu halafu umbali mrefu.

"Aliacha watoto sita na mke mwenzangu alipofika hospitali ya wilaya, alijifungua lakini mtoto alifariki dunia alizaliwa akiwa kachoka. Mimi nina watoto sita, wakiugua, ninapata shida sana, hakuna zahanati," alisema.

"Ikiwa usiku gharama ni 30,000 huku ni porini na ni mbali kuna fisi wengi, unakuta unakaa mbali na umelala na mke wako unapigiwa simu wakati mwingine saa saba za usiku au saa nane hali hii inawashinda mabodaboda wengi mwingine akikupigia simu unaacha kupokea na wakati huo mgonjwa ana hali mbaya anakosa msaada anazidiwa anaamua kujifungulia nyumbani wengine wanakufa, au uchungu unazidi anazalia njiani,"alisema Wambura.

KUTOKA KWA MUUGUZI

Rebeka Samson, muuguzi katika Zahanati ya Mtana, anayetoa huduma ya kliniki chini ya mti kwenye Kijiji cha Nyagiswa, alisema ameamua kutoa huduma hiyo kwa kuwa ni sehemu yake licha ya kukutana na vikwazo vingi wakati wa utoaji huduma.

"Huwa tunakuja wauguzi watatu, leo (juzi) niko mwenyewe, mmoja anaumwa, mwingine yuko masomoni, tunatoa huduma ya kliniki tu kwa watoto na wajawazito inayotolewa mara moja kwa mwezi na tunahudumia wagonjwa zaidi ya 50 kama unavyoona.

"Kwa kuwa niko peke yangu, kila kitu ninafanya mimi, ninapima watoto, wajawazito na huduma ya chanjo," alisema.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Nyagisya, Waitara Kemo, alisema tayari wananchi wamechimba msingi kwa nguvu zao,
wamechanga fedha na kusomba mawe na mchanga, matofali 3,500, mifuko 30 ya saruji pamoja na kuchanga Sh. milioni moja, ili kuanza ujenzi wa zahanati.

Nipashe katika kusaka mustakabali wa tatizo hilo, ilihamia kwa Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Joseph Ngowi, ambaye alisema hakuwa na taarifa za watoto na wajawazito kupata huduma ya kliniki chini ya mti.

"Sitaruhusu huduma kutolewa chini ya mti, siku zote ofisi yangu ilikuwa inajua huduma inatolewa kwenye majengo ya shule, kama serikali ya kijiji haijajipanga kuandaa jengo kwa ajili ya huduma hiyo, wananchi watalazimika kwenda kuifuata kata jirani ya Manga kupata huduma ya kliniki katika Zahanati ya Mtana," alisema.

Ngowi alisema huo ni mwongozo wa serikali kwenye huduma na watumishi wanalifahamu hilo na kwamba muuguzi aliyetoa huduma chini ya mti, amefanya makosa.

Habari Kubwa