Wakala wa basi afariki kwa kukanyagwa na basi

27Mar 2020
Marco Maduhu
Shinyanga.
Nipashe
Wakala wa basi afariki kwa kukanyagwa na basi

Athumani Omari (38) mkazi wa Jijini Mwanza, ambaye ni wakala wa Basi la Kisbo lenye namba za usajili T 192 DBZ, amefariki dunia kwa kukanyangwa na Basi hilo kwenye Stendi kuu ya Mabasi Mkoani Shinyanga.

Tukio hilo limetokea leo majira ya 2:30 asubuhi, wakati basi hilo la Kisbo likitokea Jijini Mwanza kwenda Dar es salaam, likiwa na wakala huyo lilipofika Shinyanga kupakia abiria, na wakati likiondoka ndipo akarukia kwenye basi na kuteleza chini ya uvungu, akanyagwa na kufariki dunia papo hapo.

Akisimulia tukio hilo mmoja wa mashuhuda ambaye ni Mfanyabiashara wa Standi, Joseph Thomas, alisema wakati basi hilo likiondoka ndipo wakala huyo akaanza kulikimbilia,na alipo rukia kwenye mlango akateleza na kisha kukanyagwa na mataili.

Alisema wakati basi likiondoka hapo Stendi lilikuwa katika mwendokasi, na baada ya wakala huyo kukanyagwa, dereva wa basi alitelemka na kukimbia.

"Mimi nimeshuhudia kabisa huyu wakala wa basi akikanyangwa na basi la Kisbo, yani alipokuwa ana rukia kwenye basi akateleza mlangoni na kuangukia kwenye uvungu wa basi, ndipo akakanywa na mataili na mwili wake kusambalatishwa utumbo wote ukatoka nje," alisema Thomas.

Naye dereva wa magari kwenye Stendi hiyo ya Mabasi Shinyanga Paschal Mboje, alitoa wito kwa askari wa vikosi vya usalama barabarani kwenye Standi hiyo, wazuie Mabasi na kuyatoa kwa foleni na siyo kuruhusu kutoka hovyo, ambapo hutoka kwa mwendokasi hali ambayo ni hatari.

Kwa upande wake Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga Deborah Magiligimba, alithibitisha kutokea kwa ajili hiyo, na kubainisha mwili wa marehemu umehifadhiwa kwenye chumba cha maiti katika hospital ya Rufani mkoani humo.

Aidha alisema Dereva wa Basi hilo Jabu Dalueshi (45), ambaye ni mkazi wa Jijini Dares salaam ana shikiliwa na Jeshi la Polisi pamoja na Basi hilo.

Pia alitoa wito kwa madereva, kuwa makini pale wanapo ondoa mabasi kwenye Stand za mabasi, watumie vioo vya kuendeshea magari (Site Mirror), ili kubaini kama kuna mtu ana kimbilia basi na kuepukana na ajili zisizo za lazima. 

Habari Kubwa