Wakalia mawe kisa ukosefu madawati

19Jan 2019
Ibrahim Yassin
Tunduma
Nipashe
Wakalia mawe kisa ukosefu madawati

WANAFUNZI waliojiunga kidato cha kwanza katika Shule ya Sekondari Jakaya Kikwete, iliyoko katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma, mkoani Songwe, wanakalia mawe darasani kutokana na uhaba wa madawati.

Mbali na changamoto hiyo, pia shule hiyo inakabiliwa na ukosefu wa vyumba tisa vya madarasa na vilivyopo ni vitatu wakati mahitaji ni vyumba 13 kwa ajili ya kutosheleza mahitaji ya wanafunzi 474.
 
Tumaini David, mkazi wa Tunduma alisema jana kuwa ni aibu kwa serikali wilayani hapa kwa kuwa badala ya kufanya maandalizi mapema walisubiri hadi wanafunzi waanze masomo ndipo waanze kuhangaika.
 
''Hivi inaingia akilini kweli? Serikali inafahamu wazi kuwa kila mwaka wanafunzi wanachaguliwa kujiunga kidato cha kwanza, lakini wao hawashughuliki wanafanya harakati hizi wakati tayari muda wa masomo umeanza, wamekosea sana,” alilalamika Tumaini.
 
Gidion Siwale, mkazi wa Tunduma alisema tatizo la madawati na vyumba vya madarasa ni kubwa na kwamba wako tayari kushirikiana na serikali kutatua,b sambamba na kuweka mikakati ya pamoja ya upanuzi wa shule kuhepuka usumbufu licha ya kuwa hawajaandaliwa mapema.
 
Alisema suala la elimu ni muhimu na ilipaswa waelezwe mapema kuhusu ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kuwa wao ndio wenye shule na wangeweza kufyatua matofali, kusomba mchanga na kujenga na kwamba serikali ingefanya kazi ya kupaua lakini hilo halikufanyika.
 
Mwalimu Anna Sanga ambaye ni mkuu wa shule hiyo, licha ya kukiri wanafunzi kukaa kwenye mawe kwa kukosa madawati, alisema shule hiyo ina vyumba vitatu vya madarasa wakati mahitaji ni vyumba 12 kwa ajili ya kumudu wanafunzi 474 wa kidato cha kwanza.
 
Alisema jitihada za makusudi zinahitajika kunusuru wanafunzi hao ili waweze kusoma kwa raha pasipo kubanana na kwamba kutokana na changamoto hizo,anauhakika kuwa suala hilo litafanyiwa ufumbuzi wa haraka.
 
Kastori Msigara, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, alisema ni kweli jambo hilo lipo na kwamba halmashauri kwa kushirikiana na wadau wanafanya jitihada za haraka kuhakikisha majengo na madawati yanapatikana zinafanyika.

 

Habari Kubwa