Wakandarasi miradi ya maji wanaosingizia corona waonywa

22May 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wakandarasi miradi ya maji wanaosingizia corona waonywa

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amewaagiza wakandarasi wote walioitelekeza miradi ya maji kwa sababu ya Ugonjwa wa Virusi vya corona kurudi kwenye maeneo yao ya kazi kuendelea na utekelezaji haraka.

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akitoa onyo kwa mwakilishi wa mkandarasi Kampuni ya M/S Nangai Engineering Ltd baada ya kukagua na kutoridhishwa na maendeleo ya kazi ya ujenzi wa Mradi wa Maji wa Vijiji 6 vya Songambele, Mlowa, Majengo, Tambukareli, Zinginali na Itigi katika Halmashauri ya Itigi, mkoani Singida.

Naibu Waziri Aweso ametoa agizo hilo baada ya kukasirishwa na utendaji wa wakandarasi wa Kampuni za M/S Nangai Engineering Ltd na M/S Nipo Africa Engineering Ltd wanaosuasua katika utekelezaji wa ujenzi wa Mradi wa Maji wa Vijiji 6 vya Songambele, Mlowa, Majengo, Tambukareli, Zinginali na Itigi katika Halmashauri ya Itigi, mkoani Singida.

Amesema kuwa zaidi ya Sh. Bilioni 1.3 zimeshatolewa kwenye mradi huo na maendeleo ya kazi yakiwa nyuma ya ratiba na kukwamisha lengo la mradi unaotarajiwa kuhudumia wakazi wapatao 31,000 katika vijiji 6 vinavyozunguka mji wa Itigi.

“Kipindi hiki cha Ugonjwa wa Corona, ni haki kwa kila mtanzania kupata huduma toshelevu ya maji ili kulinda afya za wananchi dhidi ya ugonjwa huu, pia Serikali inachukua hatua madhubuti kukamilisha haraka miradi ya maji ili iweze kutoa huduma ambayo ni haki ya kila mtanzania’’, amesema Naibu Waziri Aweso.

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akitoa maalezo baada ya kukagua ujenzi wa Mradi wa Maji wa Vijiji 6 vya Songambele, Mlowa, Majengo, Tambukareli, Zinginali na Itigi katika Halmashauri ya Itigi, mkoani Singida. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwagisa.

Ujenzi wa tenki la maji na nyumba ya pampu kwa ajili ya Mradi wa Maji wa Maji wa Kintinku-Lisulile katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida.
Ujenzi wa moja ya matenki mawili ya maji yenye ujazo wa lita 200,000 kwa ajili ya Mradi wa Maji wa Vijiji 6 vya Songambele, Mlowa, Majengo, Tambukareli, Zinginali na Itigi katika Halmashauri ya Itigi, mkoani Singida.

“Nawaagiza wakandarasi wote walioitelekeza miradi ya maji kwa sababu ya Ugonjwa wa Virusi vya Corona warudi kwenye maeneo yao ya kazi na kukamilisha ujenzi wa miradi haraka, ni kweli ugonjwa upo tunachotakiwa ni kuchukua tahadhari lakini kazi zisisimame, atakayekaidi agizo la Serikali tutamchukulia hatua za kisheria kwa kuwa atakuwa anatukwamisha”, ameonya Naibu Waziri Aweso.

Amewatahadharisha wakandarasi kuacha tabia ya kuitelekeza miradi kwa muda mrefu, na kuonekana kwenye maeneo ya kazi pindi viongozi wa wizara wanapokuwa wakifanya ziara za kukagua miradi hiyo kwa lengo la kutaka kuridhisha viongozi hao.

“Niwatake watumishi wa Wakala ya Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) kuwabana wakandarasi wafanye kazi zao usiku na mchana na kutoa taarifa za mara kwa mara zinazohusu changamoto zote za kiutekelezaji ziweze kutatuliwa haraka ili miradi isikwame”, amesema Naibu Waziri Aweso 

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Manyoni, Mhandisi Gabriel Ngongi akisoma taarifa ya Mradi wa Maji wa Kintinku-Lisulile kwa Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida.
Mitambo ya kusukuma maji ya Mradi wa Maji wa Maji wa Kintinku-Lisulile katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida.

Mapema Naibu Waziri Aweso alitembelea Mradi wa Maji wa Kintinku-Lisulile katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na kuelekeza mkandarasi alipwe Sh. Milioni 370 anazodai aweze kukamilisha awamu ya kwanza ya ujenzi wa mradi huo, ambapo asilimia 10 imebaki ili uweze kukamilika.

Amesema wakati wa usomaji wa Bajeti ya Wizara ya Maji, wabunge walizungumzia sana juu ya kukamilika kwa miradi ya maji katika Wilaya za Manyoni na Itigi, na kutoa ahadi ya kutembelea miradi hiyo kabla ya Bajeti Kuu kusomwa ili kuchukua hatua za haraka za kuikamilisha.

Amesema taarifa ya Mradi wa Maji wa Vijiji 6 katika Halmashauri ya Itigi, Meneja wa RUWASA Wilaya ya Manyoni, Mhandisi Gabriel Ngongi amesema ujenzi wa mradi unasimamiwa na RUWASA, utekelezaji wake ulianza Mwezi Disemba, 2018 na unategemea kukamilika ifikapo Mwezi Juni, 2020 kwa gharama za zaidi ya Sh. Bilioni 2.6.

Amesema miongoni wa kazi za ujenzi ni ujenzi wa matenki mawili ya maji yenye ujazo wa lita 200,000, tenki la maji la lita 100,000, vituo vya kuchotea maji 40 na vioski 16 vya kutolea huduma, lambo la kuhudumia wanyama pamoja na kazi nyingine.

Habari Kubwa