Wakazi 27,332 wa vijiji sita Kagera wanufaika na mradi wa maji

19Dec 2021
Lilian Lugakingira
KAGERA
Nipashe Jumapili
Wakazi 27,332 wa vijiji sita Kagera wanufaika na mradi wa maji

WAKAZI 27,332 wa kata za Rubale na Rukoma zenye vijiji sita vilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, wameondokana na adha ya maji na kuimarisha afya za wanafunzi, baada ya utekelezaji wa mradi wa Maji wa Rukoma na elimu unaofadhiliwa na Shirika la World Vision Ujerumani na Australia.

DC Bukoba, Moses Machali akimtwisha ndoo ya maji mmoja wa wananchi.

Miradi hiyo iliyogharimu zaidi ya Shilingi milioni 518.1 iliyokabidhiwa kwa serikali na jamii husika ambayo itachukua jukumu la kuisisimamia, kuilinda na kuiendeleza kwa ajili ya ustawi wa jamii hasa watoto.

Akikabidhi miradi hiyo Kaimu Meneja wa Shirika la World Vision Kanda ya Kagera, Victor Nsiima alimweleza Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Moses Machali kuwa miradi hiyo inavihudumia vijiji vya Rubale, Kabirizi, Migara, Rukoma, Bituntu na Nsheshe.

Nsiima, alisema mradi wa maji wa Rukoma umefanikiwa kujenga mradi mkubwa wa maji unaotumia nguvu ya umeme wa jua wenye jumla ya vituo vitatu katika kijiji cha Nsheshe uliogharimu zaidi ya Shilingi milioni 178.9.

"Pia limejengwa tangi la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 50,000 katika Shule ya Msingi Bunywambele uliogharimu zaidi ya Shilingi milioni 37.3, uchimbaji wa kisima kirefu cha maji katika kijiji cha Kabilizi kilichogharimu zaidi ya Shilingi milioni 35.5 na ujenzi wa mfumo wa kunawia mikono katika shule ya msingi Ruzila uliogharimu Shilingi milioni 16" alisema Nsiima.

Alisema kuwa pia wamejenga  vyoo vitatu katika shule ya Bitutu na Bunywambele vyenye jumla ya matundu 14 vilivyogharimu zaidi ya shilingi  mil. 66.1.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Moses Machali aliwashukuru shirika la World Vision kwa kuisaidia serikali kutekeleza miradi ya maji na elimu katika kata hizo ambazo zilikuwa zinakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji kwa muda mrefu na upungufu wa vyumba vya madarasa na vyoo. Alisema jukumu la jamii kwa sasa ni kuitunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu, na kwamba hilo litafanikiwa endapo wazazi na walimu watawafundisha watoto wao kuwa wasafi na waadilifu.

Aidha aliwataka viongozi wa kamati ya maji ya Karama kijiji Nsheshe waliopewa jukumu la kusimamia mradi huo kuwa waaminifu kwa kuepuka ubadhilifu wa fedha zinazochangwa na wanakijiji kwa ajili ya kuendeleza mradi huo.

Kwa upande wake Meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Wilaya ya Bukoba, Mhandisi EVarist Mgaya alisema baada ya mradi kukamilika umeanza kutoa maji katika visima hivyo ambavyo vitahudumia watu zaidi ya 1,200  wa Kijiji cha Nsheshe lakini akadai kuwa  wanatarajia kuutanua katika vijiji vingine jirani ili kuondoa kabisa tatizo la katika maeneo hayo.

Mmoja wa wananchi wa kijiji cha Nsheshe, Simon Binamungu alisema kuwa wameanza kunufaika na mradi huo wa maji kwa kuanzisha kilimo biashara kwa lengo la kujiinua kiuchumi.

Mradi wa World Vision Rukoma AP ulianza utekelezaji wa shughuli zake mwaka 2019 na umekuwa ukijishughulisha na miradi ya afya, maji,  usafi, elimu na ufadhili wa watoto.

Habari Kubwa