Wakazi 346,365 Itilima kunufaika ujenzi wa Hospitali

24May 2019
Happy Severine
ITILIMA
Nipashe
Wakazi 346,365 Itilima kunufaika ujenzi wa Hospitali

Jumla ya wakazi wapatao 346,365 wa Wilaya ya Itilima na maeneo ya jirani wanatarajia kunufaika na ujenzi wa mradi wa hospitali ya Wilaya ya Itilima inayotarajiwa kukamilika juni 30 mwaka 2019.

moja ya jengo la hospitali ya Wilaya ya Itilima Mkoani Simiyu,likiwa katika hatua za ujenzi.

Mradi huo wenye lengo la kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya na kusogeza karibu huduma hiyo kwa wananchi ,hadi kukamilika kwake unatarajia kutumia kiasi cha sh bil 1 .5.

Akisoma taarifa ya mradi wa Ujenzi wa Hospital ya Wilaya ya Itilima leo kwa kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru mwaka 2019,Mzee Mkongea Ali ,mganga mkuu wa Wilaya hiyo Dk Anorld Charles amesema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha huduma za  wananchi wa Wilaya humo.

Dk Charles ameeleza kuwa wananchi wengi wa Wilaya hiyo wamekuwa wakitembea umbali mrefu wa wastani wa kilometa 45 hadi 50 kufuata huduma za afya katika hospitali ya Bariadi.

Amesema kutokana na hali hiyo ya kutembea umbali mrefu,wengi wao hupoteza maisha kwa kukosa huduma stahiki za haraka hususani akinamama wajawazito ambao wengi wao hupoteza damu nyingi njiani.

Ameongeza kuwa endapo hospitali hiyo itakamilika kwa muda muafaka,itasaidia sana kupunguza vifo vya akinamama wajawazito wanaopoteza damu nyingi pindi wawapo njiani kuelekeza katika hospitali ya wilaya ya Bariadi.

Amesema kwa mwaka 2018 (Jan hadi Dec) pekee jumla ya akinamama 5 walipoteza maisha kwa kuvuja damu nyingi kwa kucheleweshwa kufika mapema katika zahanati na hospitali zilizo karibu nao.

Nae kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa Mzee Mkongea alisema kuwa jitihada za Ukamilishaji wa hospitali hiyo zinatakiwa ziwe za haraka iwezekanapo kabla ya kuisha mwaka wa fedha, kwani endapo wakishindwa kukamilisha kwa muda husika hawataweza kupata fedha za ukamilishaji huo.

" napenda kuwashauri kuwa ukamilishaji wa hospitali hiyo unatakiwa uwe junior 30, mwaka huu hivyo ni lazima ujenzi uende kwa haraka usiku na mchana...la sivyo mwaka ya fedha 2018/2019 utakapomalizika itakuwa vigumu kupata fedha hizo zilizokuwa zimetengwa katika bajeti ya 2018/2019.

Nae Marangwa Maduhu mkazi wa kijiji cha Nguno Wilayani humo,amesema uwepo wa hospitali hiyo itawasaidia sana kupunguza gharama za usafiri walizokuwa wakizitumia kufuata matibabu Wilayani Bariadi.

Mpaka sasa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Itilima tayari imeshatumia kiasi cha sh bil 1.2 sawa na asilimia 81 ya utekelezaji wake.

Habari Kubwa