Wakazi Dar, Pwani wahakikishiwa maji ya uhakika

07Jul 2019
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wakazi Dar, Pwani wahakikishiwa maji ya uhakika

Afisa Mtendaji Mkuu wa Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja ameweka wazi kuwa tatizo la maji ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam na Pwani linaenda kuisha.

Afisa Mtendaji Mkuu wa Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprian Luhemeja akisaini kitabu Cha wageni baada ya kutembelea Banda la dawasa katika maonyesho ya Saba saba Leo.

Luhemeja ameyasema hayo alipotembelea banda la DAWASA lilipo ndani ya maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na wanahabari baada ya kupata maelezo kutoka kwa watoa huduma kwa wateja na wahandisi, Luhemeja amesema shida ya maji ndani ya mkoa wa Dar es Salaam na Pwani inaelekea kuisha kutokana na miradi mbalimbali inayoendelea kujengwa na ile mipya.

Luhemeja amesema, wameshasaini miradi mikubwa sita ya maji yenye thamani ya bilion 114.5 ambapo itasambaza maji ndani ya mkoa wa Dar es Salaam na Pwani.

"Wananchi walikua na shida ya maji na miradi hii mikubwa inaenda kuondoa changamoto ya maji na malengo kufikia asilimia 95 mwaka 2020," amesema Luhemeja.

Amesema, kwa sasa maji yanapatikana kwa asilimia 85 tofauti na miaka ya nyuma ambapo maji yalikua asilimia 68 na mapato yamepanda kutoka bilion 3.2 kwa mwezi hadi bilioni 11.2.

Akielezea sheria mpya namba 5 ya mwaka 2019 inayoibadilisha mamlaka ya majisafi na majitaka na kuwa mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira, Luhemeja amesema wameipokea vizuri na itasaidia katika kulinda vyanzo vya maji na kudhibiti usafi wa mazingira.

Aidha, Luhemeja amesema DAWASA bado wanaendelea na kusajili wamiliki wa Visima na kuhakiki ubora wa maji na kuwajua kutokana na sheria mpya kuwaondolea kodi ya kila mwaka.

Ametoa rai kwa wananchi kufika kwenye banda lao lilipo ndani ya maonesho ya 43 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba kwenye Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Jijini Dar es Salaam ili kufahamu miradi ya maji inayoendelea kujengwa na mipya itakayoondoa changamoto ya maji ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Imeandikwa na Zainab Nyamka na Cathbert Kajuna