Wakazi wa Changanyikeni kusahau shida ya maji rasmi

25Nov 2018
Na Mwandishi Wetu
Dar es salaam
Nipashe Jumapili
Wakazi wa Changanyikeni kusahau shida ya maji rasmi
  • Ni baada ya tenki la Changanyikeni kujazwa maji kesho
  • Mpaka siku ya Jumatano wananchi watakuwa wameunganishiwa maji

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Umwangiliaji Mhadisi Emmanuel Kalobelo amesema kuanzia kesho Novemba 26 wakazi wa Changanyikeni wataondokana na shida ya Maji baada ya tenki la Maji la eneo hilo kuanza kupokea maji na kufikia Jumatano wananchi watakuwa tayari wameshaunganishiwa maji.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji Mhandisi Emmanuel Kalobelo (kushoto) akipata maelezo ya mradi kutoka Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) Mhandisi Cyprina Luhemeja (wa pili kushoto) akiwa sambamba Mkurugenzi wa Maji na Usafi wa Mazingira wa Wizara ya Maji na Mjumbe wa Bodi ya DAWASA Mhandisi Nadhifa Kemikimba, Mkurugenzi wa Miradi wa DAWASA Mhandisi Lydia Ndibalema.

Hayo ameyasema leo wakati wa ziara ya kukagua miradi ya upanuzi wa huduma ya maji inayotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka (DAWASA) inayohusisha ujenzi wa matenki na upanuzi wa mtandao.

Miradi hiyo itanufaisha Manispaa za Kinondoni na Ubungo na Halmashauri ya Mji wa Bagamoyo ukiwa unahusisha matenki matano yenye ujazo wa Lita Milioni 6.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mhandisi Kalobelo amesema mradi huu ulio mbioni kukamilika umeanza kuonesha manufaa kwa wananchi wa Changanyikeni kuanza kupata maji.

Mhandisi Kalobelo amesema, matarajio ya serikali ni kuona wananchi wanapata maji safi na salama na maji ni rasilimali adimu wananchi wanatakuwa watunze miundo mbinu.

Amesema, kulikuwa na malalamiko kutoka kwa wananchi wa Goba, Wazo, Changanyikeni na Salasala ya kukosa maji kwa muda mrefu ila kumalizika kwa miradi hii mikubwa iliyowezeshwa na serikali kupitia Wizara ya Maji wananchi wataanza kunufaika baada ya kuyasubiri maji kwa muda mrefu.

" mradi huu ni wa awamu ya kwanza, kuna mradi wa pili ambao serikali tayari imepata hela kutoka Benki ya Dunia utakaowanufaisha wananchi walio maeneo ambayo hajayanufaika na mradi kwa kwanza," amesema Mhandisi.

Amewapongeza DAWASA kwa jitihada wanazozionyesha kwa kuhakikisha wananchi wanapata maji na ametoa rai kwa wananchi wajiunge kwenye mradi huu ili wapate maji safi na salama.

Habari Kubwa