Wakazi wa Majohe kusahau kero ya maji, maji ya visima basi

18Mar 2019
Frank Monyo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wakazi wa Majohe kusahau kero ya maji, maji ya visima basi

WAKAZI zaidi 7,000 wa mtaa wa Kichangani Kata ya Majohe, Wilayani Ilala, Jijini Dar es Salaam, wanatarajia kuondokana na adha ya maji ifikapo Aprili 30, mwaka huu, utakapokalika mradi wa maji na tanki la kuhifadhia maji lita 150,000.

Katibu Tawala, Sheila Lukuba, akizungumza na wananchi wa majohe kabla ya kuzindua mradi huo.

Mradi huo unatekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA)   kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ilala kwa gharama ya Sh. milioni 229.7 kwa lengo la kuondoa kero hiyo kwa wananchi na  magonjwa yanayotokana na ukosefu wa huduma ya majisafi na salama.

Mkuu wa Idara ya Maji Manispaa ya Ilala, Mhandisi Upendo Lugongo, akitambulisha mradi huo kwa wakazi wa eneo hilo leo, amesema mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi SK Bulding and Civil Engineering Work na watajenga vituo saba vya kuchotea maji na kukamilika mwisho wa mwezi Aprili mwaka huu.

Amesema mbali na mradi huo pia wanatekeleza mradi mkubwa wa maji kutoka wilaya ya Kisarawe ambao utawezesha kata yote ya Majohe kupata maji ya uhakika.

“Ifikapo mwisho wa mwaka huu, maeneo mengi ya kata ya Majohe watakuwa wameshapata maji ya uhakika kwa sababu kuna mradi mkubwa wa maji unaojengwa Wilayani Kisarawe utawezesha maji kupatikana kwa wingi," amesema Lugongo.

Kwa upande wake mgeni rasmi katika uzinduzi huo, Mkuu wa wilaya ya Ilala, Sophia Mjema, aliyewakilishwa na Katibu Tawala, Sheila Lukuba, aliwasihi wananchi hao kuutunza mradi huo ili uwanufaishe na vizazi vijavyo.

Pia alitaka wananchi hao kulipa bili za maji ili DAWASA waendelee kuimarisha kuhuduma za maji katika jiji hilo hasa katika kipindi hiki cha wiki ya maji yenye kauli mbiu inayosema 'Hakuna atakayeachwa kuongeza kasi ya upatikani wa huduma ya majisafi na usafi wa mazingira kwa wote katika dunia inayobadilika kitabia nchi'.

“Maji haya ni ya bomba na safi na salama lakini mkumbuke kuyachemsha na kuepuka magonjwa ya milipuko kama kuharisha na kipindupindu," amesema Mjema.

 

Habari Kubwa