Wakazi zaidi ya 100 wafundishwa ufugaji wa jongoo bahari Mtwara

14Jan 2022
Abdallah Khamis
MTWARA
Nipashe
Wakazi zaidi ya 100 wafundishwa ufugaji wa jongoo bahari Mtwara

MKUU wa Wilaya ya Mtwara, Dunstan Kyobya, amewataka wakazi wa mkoa huo kutumia fursa ya ufugaji wa jongoo wa baharini  kwa kile alichoeleza samaki hao wana bei nzuri katika soko ambapo kilo moja ya samaki hao huuzwa Shilingi 180,000.

Baadhi ya washiriki wa Mafunzo ya ufugaji Samaki wakimsikiliza mtoa mada(haonekani pichani),wakati Mafunzo hayo yakiendelea Mkoani Mtwara.

Kyobya ametoa kauli hiyo mkoani humo wakati akifungua mafunzo ya muda mfupi ya ufugaji samaki yaliyowahusisha wakazi zaidi ya 100 kutoka makundi ya wanasiasa, wakulima wafanyabiashara na watumishi wa umma mkoani Mtwara.

Katika ufunguzi wa mafunzo hayo ya siku 10, yanayofanyika katika Manispaa ya Mtwara Mikindani na kufadhiliwa na Wakala Elimu na Mafunzo ya Uvuvi (FETA), iliyo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Kituo cha Mikindani.

Kyobya amesema ni jambo la kusikitisha kuona watu wengi wa Mtwara hawazitumii ipasavyo fursa zinazowazunguka na badala yake fursa hizo zinatumiwa na watu kutoka nje ya mkoa huo.

“Ufugaji wa samaki haumzuii mtu kufanya shughuli zingine za maendeleo, muhimu ni kujiwekea malengo ninawahakikishia mkizingatia haya mafunzo na mkaenda kufanyia kazi ipasavyo,mtapiga hatua kubwa kiuchumi tofauti na ilivyo sasa”amesema Kyobya.

Amesema utafiti alioufanya katika Wilaya ya Mtwara iliyozungukwa na bahari,kuna baadhi ya samaki wanauzwa kwa bei ya juu huku wavuvi na wafugaji wakiwa hawajielekezi kufuga aina hiyo ya samaki.

"Juzi nimefika kwa muuza samaki anauza wale samaki kamba ndoo ya kilo 10 kaniambia ataniuzia kwa shilingi 250,000 na hapo ndiyo amenionea aibu mimi mkuu wa wilaya sasa je mkiwa na uhakika wa kufuga samaki wa aina hiyo kwa wingi si mtakuwa mmeachana na umasikini” amehoji Kyobya

Kaimu Meneja Kampasi ya  Mikindani, Isac Tarimo, amesema kwa sasa kituo hicho kinatoa mafunzo ya muda mfupi kwa watu mbali mbali ikiwa ni maandalizi ya kutoa mafunzo ya muda mrefu, mara majengo ya kufundishia yatakapokamilika.

“Hadi sasa Kampasi ya Mikindani imetoa mafunzo ya mbinu bora za ufugaji samaki kwa wakazi wa Mtwara na maeneo jirani ambapo watu 113, walitunukiwa vyeti vya ushiriki. Pia, tumefanikiwa kufadhili mafunzo ya ufugaji wa samaki katika maji baridi kwa wakazi wa Mtwara ambayo tunayaendesha kuanzia tarehe 13 hadi 26 Januari 2022.”amesema Tarimo

Ameongeza kuwa katika mafunzo hayo wamepanga  kuendesha mafunzo ya mbinu bora za ufugaji wa samaki na mazao ya baharini yatakayojumuisha ufugaji wa jongoo  wa baharini, Sato wa maji chumvi na maji baridi, pamoja na namna bora ya uchimbaji wa mabwawa ya kufugia.

Habari Kubwa