Wakenya jela miaka minane kwa wizi

12Jan 2017
Samson Chacha
Nipashe
Wakenya jela miaka minane kwa wizi

RAIA wawili kutoka Wilaya ya Kurya nchini Kenya,wamehukumiwa kifungo cha miaka minane jela baada ya kupatikana na hatia ya kuvunja na kuiba vifaa vya umeme vyenye thamani ya Sh. 849,000.

Walihukumiwa kutumikia kifungo hicho ambapo kila mmoja atafungwa miaka minne, ni Lucas Chacha (25) na Mohere Chacha (28).

Vifaa vya umeme walivyoiba ni betri na sola vilivyokuwa vikitumika katika Shule ya Msingi Nyakarima iliyopo Kata ya Ganyange wilayani hapa.

Hukumu hiyo ilitolewa na Hakimu wa mahakama hiyo, Amon Kahimba, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka uliongozwa na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Mwanri Mrisho.

Awali, ilidaiwa na Mwendesha Mashtaka Mrisho kuwa Oktoba 24, mwaka juzi, washtakiwa hao kwa pamoja walivunja stoo ya Shule ya Msingi Nyakarima iliyopo katika Kata ya Ganyange wilayani Tarime na kuiba vifaa vya umeme ikiwamo sola moja yenye thamani ya Sh. 800,000 na betri yenye thamani ya Sh. 49,000 iliyokuwa ikitumika kuwasha sola hiyo vyote vikiwa na thamani ya Sh. 849,000.

Hata hivyo, washtakiwa hao walikana shtaka hilo.

Upande wa mashtaka ulileta mashahidi wanne huku upande wa watuhumiwa wakishindwa kupeleka mashahidi.

Wakijitetea, washtakiwa hao waliiomba mahakama iwape adhabu ndogo kwa kosa wakidai wana familia zinazowategemea wakiwamo watoto mahakama hiyo kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hiyo.

Hakimu Kahimba aliungana na upande wa mashtaka na kuwahukumu kila mmoja kwenda jela miaka minne.

Habari Kubwa