Wakili adai namba ya mshitakiwa kesi ya Mbowe imeuzwa kwa mtu

15Jan 2022
Kulwa Mzee
Dar es Salaam
Nipashe
Wakili adai namba ya mshitakiwa kesi ya Mbowe imeuzwa kwa mtu

WAKILI wa utetezi katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), John Mallya, ameibua jambo mahakamani baada ya kudai kuwa laini ya simu ya mshtakiwa wa kwanza, Halfan Bwire, imeuzwa kwa mtu mwingine.

Mallya aliibua madai hayo jana katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi wakati akimhoji Mwanasheria wa Airtel, Gladys Fimbari, huku akidai kuwa namba hiyo aliyochunguza miamala, imeuzwa kwa mteja mwingine, Godson Munuo  kwa Sh. 500.

Mallya alimbana maswali shahidi huyo mbele ya Jaji Joackim Tiganga wakati akitoa ushahidi kuhusu Luteni Dennis Urio mwenye namba 0787 555200 aliyetumiwa Sh 500,000 na Mbowe kwamba alitoa Sh. 300,000.

Alidai kuwa kumbukumbu yoyote aliyotoa mahakamani kuonyesha Sh. 80,000 zilizotumwa kwa namba inayodaiwa ya Bwire ilikwenda wapi.

Akihojiwa shahidi alidai line za Airtel wanauza kwa Sh. 500 na alipotakiwa kueleza kama anajua namba ya Bwire 0782 237913 kwa sasa imeuzwa kwa Godson Munuo kwa Sh 500, alidai hakujua kama imeuzwa.

Kuhusu fedha zilizokuwa katika namba hiyo ya simu, alidai zinawekwa katika akaunti ya kukusanya fedha.

Pia shahidi huyo alihojiwa na Wakili Peter Kibatala, anayeongoza jopo la kumtetea Mbowe na wenzake na kuulizwa kama anafahamu kuwa Mbowe ni Mwenyekiti wa CHADEMA na kwamba anashtakiwa kwa ugaidi.

Shahidi huyo alidai kuwa wanatakiwa kulinda haki za mteja na kwamba mteja kwao ni mtu muhimu, hivyo wanaangalia sana taarifa zake lakini pale panapohitajika kisheria wanafuata sheria kutoa taarifa hizo.

"Hakuna sheria inayokataza kuhoji amri ya kuwataka kutoa taarifa za mteja. chombo kilichoomba taarifa za wateja kinaruhusiwa kisheria kupewa.

"Wakati natafuta taarifa za miamala kwa namba ya Mbowe, nilijua namba yake kwa sababu niliona aliyesaini (aliyetia saini) barua ya kuomba taarifa za namba za simu simjui. Barua ilikuwa na namba ya simu lakini sikuipiga isipokuwa baada ya wiki moja nilikwenda kutoa maelezo Polisi,"alidai shahidi.

Alidai kuwa barua iliyokwenda Airtel ilielekezwa kwa mwanasheria lakini hakuieleza mahakamani barua hizo zinahifadhiwa wapi na wala hakusema polisi ilifikaje.

Fimbari alidai barua ya kuomba taarifa za miamala ilimfikia Julai 2, mwaka jana, na siku hiyo hiyo aliifanyia kazi na kujibu lakini hakusema kwa nini aliifanya kazi hiyo kwa haraka.

Alidai kuwa Airtel walikuwa hawafahamu kama Mbowe anashtakiwa kwa ugaidi kwa kuwa barua ilieleza taarifa hizo zinahitaka kwa ajili ya makosa ya jinai.

Shahidi huyo wa tisa alimaliza kutoa ushahidi, hivyo upande wa Jamhuri unatarajiwa kuleta shahidi wa 10 katika kesi hiyo na hadi sasa bado mashahidi 15 watakaotoa ushahidi kwa upande wa mashtaka na kufanya mashahidi kuwa 24..

Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mbowe, Bwire, Adamu Kasekwa na Mohammed Ling'wenya ambao wanashtakiwa kwa kula njama kufanya vitendo vya kugaidi kati ya Mei Mosi na Agosti 5, 2020.

Wanadaiwa kutaka kufanya matukio hayo yakiwamo maandamano yasiyo na ukomo, kulipua vituo vya mafuta na kukata miti.

Habari Kubwa