Wakili kutoa ushahidi kesi kughushi

20Oct 2021
Kulwa Mzee
Dar es Salaam
Nipashe
Wakili kutoa ushahidi kesi kughushi

WAKILI wa kujitegemea Jerome Msemwa anatarajia kutoa ushahidi katika kesi ya kughushi cheti cha ndoa, inayomkabili Khairoon Jandu, Novemba Mosi, mwaka huu.

Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele Hakimu Mkazi Mwandamizi Joseph Lwambano na juzi, ililetwa kwa ajili ya usikilizwaji, lakini ilikwama kwa sababu wakili wa mshtakiwa huyo Abubakar Salim, alikuwa na udhuru.

Kwa mujibu wa taarifa iliyofikishwa mahakamani hapo, wakili huyo alikwenda kuhudhuria kesi, Mahakama Kuu Kitengo cha Ardhi.

Wakili wa serikali Ashura Mzava alimlalamikia wakili huyo wa utetezi akidai ni mara ya tano sasa kesi hiyo, imeshindwa kuendelea kutokana na yeye kutofika mahakamani.

"Mheshimiwa hakimu pamoja na wakili kuleta taarifa hii, lakini naona kama kuna mchezo anafanya, hii ni mara ya tano sasa kesi imeshindwa kuendelea kwa yeye kutofika mahakamani, aseme basi ni tarehe zipi atakuwapo mahakamani mimi naandaa mashahidi, lakini wakili haonekani mahakamani," alidai Wakili Mzava.

Baada ya kueleza hayo, mshtakiwa Khairoon aliieleza mahakama kuwa wakili wake amesema atafika mahakamani Novemba mosi, pili na tatu.

Hakimu Luambano alisema kesi hiyo itaendelea kusikilizwa mfululizo katika tarehe hizo na kumtaka mshtakiwa Khairoon amweleze wakili wake afike mahakamani, bila kukosa katika tarehe zilizopangwa.

Mahakama ilimuonya shahidi namkumtaka pia afike mahakamani Novemba mosi, mwaka huu.

Katika kesi hiyo, Khairoon anadaiwa kuwa katika tarehe na mwezi usiofahamika mwaka 2020, ndani ya Mkoa wa Dar es Salaam, kwa nia ovu, alighushi cheti cha ndoa. 

Ilidaiwa kwamba alighushi cheti hicho akionesha kuwa ni halali kimetolewa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA), wakati akijua si kweli.

Katika shtaka la pili, inadaiwa mshtakiwa huyo alighushi cheti cha kuzaliwa cha Gurditsingh Jandu akionesha ni halali kimetolewa na RITA wakati akijua si kweli.

Habari Kubwa