Wakili Mkuu afunguka utawala wa sheria

07Aug 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Wakili Mkuu afunguka utawala wa sheria

WAKILI Mkuu wa Serikali, Gabriel Malata, amesema ofisi yake iko makini kuhakikisha utawala wa sheria unaimarika na kwamba haitasita kupeleka rufani katika mahakama za juu kwa ajili ya kupata nafuu nyingine wanapoona sheria zinakiukwa.

Kadhalika, amesema ofisi yake ina wajibu na jukumu la kusimamia na kuhakikisha sheria zinafuatwa ikiwamo kuzingatia wajibu na haki zake.

Rai hiyo aliitoa jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

"Ofisi yangu ina haki ya kusimamia utawala wa sheria na haitasita kufungua rufani mahakama za juu kwa sababu tuna wajibu wa kusimamia na kuhakikisha sheria husika zinafuatwa," alisema na kuongeza:

"Nasikitika kuona baadhi ya mawakili ambao wanapinga maamuzi ya Mahakama nchini kwamba inashindwa kusimamia katiba, sisi mawakili tunafahamu njia za kufuata pale tunapohitaji nafuu ya mahakama na si kudhihaki na kuitusi kwenye mitandao ya kijamii au vyombo vya habari.”

Alisema mawakili wajibu wao ni kuisaidia mahakama na si kuibeza bila kujiingiza katika mivutano ya muhimili huo na endapo hawajaridhishwa na maamuzi wakate rufani au watafute namna ya kuomba nafuu kwa mujibu wa sheria.

Aliongeza kuwa kama jamii inadai sababu za kupelekwa kwa maombi hayo ni ubambikiziwaji wa kesi, lazima uwapo ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai hayo, na kwamba katika kesi hiyo hoja hiyo haijazungumzwa.

Aidha, alisema katiba kama sheria mama inapaswa kutafsiriwa kwa mapana yake kwa kuzingatia malengo, maudhui yake katika kulinda haki ya kila mtu na jamii kwa ujumla na kwamba ikitafsiriwa bila kuhusisha sheria nyingine ni rahisi kuleta sintofahamu katika jamii.

Alisisitiza kuwa utaratibu wa kuzuia dhamana ni wa kikatiba kwani wakati ibara ya 15(1) ya katiba inampa mtu haki ya kuwa huru na kuishi kama mtu huru, ibara ya 15 (2) inaruhusu haki na uhuru wa mtu kuingiliwa kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria lengo ni kulinda haki na usalama wa jamii.

Habari Kubwa