Wakili wa Kisena ahoji upelelezi kutokamilika

12Jun 2019
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Wakili wa Kisena ahoji upelelezi kutokamilika

UPANDE wa utetezi katika kesi inayowakabiliwa wanafamilia wawili,  Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (Udart), Robert Kisena (46), -

Mkurugenzi wa Kampuni ya Mabasi yaendayo Haraka Dar es Salaam (Udart), Robert Kisena akiingia mahakamani. picha: maktaba

mke wake Frorencia Mshauri maarufu Frolence Membe (43) na wenzao watatu, umeiomba mahakama kuushinikiza upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi haraka.

Kisena na wenzake wanakabiliwa  na kesi ya uhujumu uchumi, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Sh. bilioni 2.4  kwa kampuni hiyo.

Wakili wa utetezi, Peter Bethuel, alitoa malalamiko hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Augustine Rwizile katika kesi hiyo ilipopangwa kwa ajili ya kutajwa.

Wakili wa Serikali, Esther Martin alidai kuwa kesi hiyo imepangwa kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wake haujakamilika.

Madai hayo yalimfanya wakili wa utetezi kusimama na kudai kuwa kesi hiyo ni ya muda mrefu na kwamba upande wa Jamhuri unachelewesha kesi makusudi.

"Mheshimiwa Hakimu, mahakama iushinikize upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi ili haki itendeke kwa  pande zote mbili," alidai wakili wa utetezi.

Akijibu hoja za utetezi, wakili Martin alidai kuwa washtakiwa wanapaswa wawe wavumilivu na upelelezi utakamilika muda si mrefu.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Hakimu alisema  mahakama yake inapanga kesi hiyo kutajwa tena Juni 24, mwaka huu.

Awali, Wakili wa Serikaki, Glory Mwenda, alidai kuwa washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka manne ya utakatishaji wa fedha, manne ya kutoa nyaraka za uongo, manne ya kughushi, mawili kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kusababisha hasara.

Mbali na Kisena na mkewe, washtakiwa wengine katika hiyo ni Kulwa Kisena (33), Charles Newe (47) na Chen Shi (32).

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa  kuwa kati ya oktoba 2012 mpaka Mei 31, 2018 washtakiwa wanadaiwa kutenda makosa hayo.

Habari Kubwa