Wakosa huduma ya vyoo deni la umeme mil. 3.6/-

26Jan 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wakosa huduma ya vyoo deni la umeme mil. 3.6/-

SHULE ya Msingi Tandale Magharibi, Dar es Salaam, imejikuta katika wakati mgumu na wanafunzi wake kushindwa kutumia vyoo vipya vilivyojengwa kutokana na kukosa maji baada ya malimbikizo ya deni la umeme la Sh. milioni 3.6.

wanafaunzi wakipanga mstari kwenda chooni. picha:mtandao

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo yenye wanafunzi 1,195, Doris Misigaro, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa changamoto hiyo ya deni imesababisha wanafunzi kuendelea kutumia vyoo vya zamani ambavyo si rafiki kwao.

“Fedha ambazo tunapewa kila mwezi na serikali hazihusiani na masuala ya ulipaji umeme na hapa tunatumia maji ya kisima ambayo ili tuyapate tunatakiwa kuyavuta kwa pampu kwa kutumia umeme ambao tumekatiwa kutokana na deni hili la Sh. milioni 3.6,” alisema.

Alisema Tanesco waliwaeleza ili kuendelea na huduma hiyo, wanatakiwa kila mwezi kupunguza deni, kitendo ambacho hadi sasa wameshindwa kutekeleza kutokana na ukosefu wa fedha.

Mwalimu mkuu huyo alisema deni hilo la umeme ni la muda mrefu na limewaathiri watoto kwa kushindwa kutumia vyoo vipya ambavyo vimejengwa shuleni hapo na kuachana na vile vya zamani.

Nipashe ilishuhudia vyoo vya wanafunzi na walimu ambavyo vinatumika hivi sasa havipo kwenye hadhi huku vile vipya vimeshindwa kutumika kutokana na kuhitaji maji mara mtu anapomaliza kupata huduma ndani yake.

Alitaja changamoto nyingine shuleni hapo kuwa ni ya uzio na kueleza kuwa shule hiyo iko pembezoni mwa barabara na pindi wanafunzi wanapokuwa darasani wamekuwa wakishindwa kusoma vizuri kutokana na mazungumzo ya wapita njia na kelele za magari.

“Kama unavyoona wakati mwalimu yupo darasani anafundisha mara unasikia ‘Juma andazi hili hapa’ sasa hapo unaona kabisa namna watoto wanavyovurugwa na mazungumzo ya nje ataangalia nje kuona andazi au kumsikiliza mwalimu,” alisema.

Alisema wanaamini shule hiyo ikiwekewa uzio utasaidia kuondokana na changamoto hizo na kuondoa mwingiliano wa wapita njia shuleni hapo.

Habari Kubwa