Wakulima 300,000 pamba wakumbukwa

28Feb 2020
Na Mwandishi Wetu
Simiyu
Nipashe
Wakulima 300,000 pamba wakumbukwa

WAKULIMA zaidi ya 300,000 wa pamba nchini wakiwamo wa Mkoa wa Simiyu wameahidiwa fursa ya kufunguliwa akaunti za benki kwa ajili ya matumizi ya msimu huu wa zao hilo.

Ahadi hiyo imetolewa na Benki ya NMB, na kwamba imeanza mchakato wa kuwafuata wakulima wote waliopo maeneo ya vijijini na kuwafungulia akaunti bila gharama yoyote kwa ajili ya kuhakikisha katika msimu wa mwaka huu hawapati usumbufu wa kupokea malipo yao.

Hayo yalisemwa jana na Meneja wa Benki hiyo, Kanda ya Magharibi, Sospeter Magesse, wakati akizungumza kwenye mkutano wa majadiliano ya kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wa mkoa huo uliongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki.

Alisema kuwa mpango ambao wamejiwekea watahakikisha wanawafikia wakulima wote kwa haraka kabla ya msimu mpya wa kuanza kuuza pamba haujafika Juni, 2020.

Aliongeza kuwa kutokana na serikali kusisitiza msimu wa mwaka huu wakulima watalazimika kufungua akaunti benki na malipo yao yatafanyika kwa njia ya benki, NMB imejipanga kuhakikisha inafanikisha jambo hilo.

Aidha, Magesse alisema kuwa benki yake imejizatiti katika kuboresha sekta ya kilimo nchini, kwani imekuwa ikiwawezesha mikopo mbalimbali wakulima wa mazao ya kimakakati zaidi ya milioni moja.

“Tumeendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha kilimo hapa nchini, kama benki kubwa nchini tumewasaidia wakulima katika mazao ya kimkakati kama pamba, korosho, kahawa, tumbaku na mazao mengine ya chakula kama mahindi,” alisema meneja huyo.

Aliwataka wafanyabiashara hao kuitumia benki hiyo katika huduma mbalimbali za kifedha kwani ni benki yao kutokana na serikali kumiliki hisa asilimia 30, huku akiwahakikishia mikopo yenye riba nafuu.

Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Antony Mtaka, aliitaka NMB kuhakikisha inakamilisha zoezi la kuwafungulia akaunti wakulima kwa haraka na wakati kwani msimu mpya wa ununuzi wa pamba umewadia.

Mtaka alisema kuwa serikali imetoa maagizo kuwa wakulima wote wanatakiwa kufungua akaunti kwani malipo yao yatalipwa kwa njia ya benki, hivyo aliitaka benki hiyo kuhakikisha inawafuata wakulima walipo na kuwafungulia.

Habari Kubwa