Wakulima karafuu wajazwa noti

17May 2018
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Wakulima karafuu wajazwa noti

TANI 8,533.65 za karafuu zenye thamani ya Sh. bilioni 119.4,  zimenunuliwa na Shirika la Biashara la Taifa la Zanzibar (ZSTC), kutoka kwa wakulima wa zao hilo visiwani Zanzibar.

Karafuu hizo zimenunuliwa katika kipindi cha msimu wa zao hilo mwaka  2017 /2018, ambapo tani 290.88  zilinunuliwa Unguja na tani 8,242.76 kisiwani Pemba, kiasi hicho kimevuka lengo.

Alisema makadirio ya kununua zao hilo lilikuwa ni kununua jumla ya tani 6,770, na kati ya hizo Pemba zilitarajiwa kupatikana tani 6,500 na Unguja 270 kwa mwaka huu.

Akitoa mada kuhusu tathmini ya utekelezaji wa kazi za msimu wa mavuno ya karafuu kwa mwaka 2017/2018, Mkurugenzi Masoko wa ZSTC, Salum Abdalla Kibe huko Mkokotoni Kaskazini Unguja katika mkutano na wakulima wa zao hilo, amesema manunuzi hayo ni sawa na asilimia 126 ya malengo yaliyowekwa.

Aidha, alisema mafanikio yaliyopatikana kwa kipindi chote hicho, yametokana na ushirikiano mzuri baina ya wakulima, masheha na wafanyakazi wa shirika hilo katika kusimamia vyema uendelezaji wa zao hilo, ili kuhakikisha linaleta tija kwa wakulima na wananchi kwa jumla.

Mkurugenzi huyo pia alisema kwa mwaka huu,  ZSTC imefanikiwa kuanzisha vituo 33 kisiwani Pemba vinavyoendelea kutoa huduma ya kununua karafuu kutoka kwa wakulima.

Hata hivyo, alisema kuwa, pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto kubwa kwa wakulima kuchanganya karafuu zao na makonyo, matende na uchafu mwingine wanapopeleka vituoni kwa ajili ya kuziuza, pamoja na kuzianika bila kuzingatia maelekezo ya kuimarisha viwango vya ubora wanayopewa na wataalamu kwa kuacha kuzianika barabarani, sakafuni na kwenye mapaa ya nyumba.

Kwa upande wake, Ofisa Masoko kutoka Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) , Abdalla Jabir Abdalla, aliwasihi wakulima wa zao hilo na masheha kutumia huduma za benki kwa njia ya simu za mikononi (Mobile Easy Pesa), kwa kuweka fedha zao.

Habari Kubwa