Wakulima korosho watwangana makonde

14Sep 2021
Stephen Chidiye
TUNDURU
Nipashe
Wakulima korosho watwangana makonde

WAKATI serikali ikitoa bure viuatilifu vya kupulizia kwa ajili ya kuua wadudu kwenye mikorosho kwa wakulima wa mikoa inayolima zao hilo, wakulima wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma, wameripotiwa kuanzisha vurugu na kutwangana makonde wakati wakigawana dawa hizo.

korosho.

Hayo yamebainika kufuatia taarifa kutoka kwenye maeneo ya vyama vya ushirika vya msingi vilivyopo katika Kata za Mlingoti Mashariki, Ngapa, Lukumbule Tinginya na Kata ya Mchangani.

Taarifa hizo ambazo zimetolewa na baadhi ya viongozi wa serikali na viongozi wa siasa, zinaeleza kuwa baadhi ya maeneo wananchi ambao siyo wakulima wa korosho walivamia maghala usiku na kuyavunja kisha kugawana dawa hizo na kwenda kuuza kwa bei ndogo kwa wakulima.

Wakizungumza na Nipashe, baadhi ya wakulima wa zao hilo walisema serikali ilipaswa kuweka kiasi kidogo cha fedha wakati wa kugawa dawa hizo, lakini kwa utaratibu wa kugawa bure imewanufaisha wakulima hewa.

Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Wilaya ya Tunduru (TAMCU), Mussa Manjaule, alithibitisha kuwapo kwa matukio hayo.

Alisema mbali na upungufu wa dawa hizo, lakini wangefuata maelekezo na utaratibu wa ugawaji wake, kwamba matukio hayo yasingejitokeza.

 

Alisema hadi sasa TAMCU kimepokea tani 1,108 za dawa ya unga aina ya Sulpher ambazo zimepokelewa pamoja na lita 179,701 za dawa ya maji zimepokelewa na kusambazwa kwa wakulima.

Alisema dawa hizo ni kati ya mahitaji ya mgawo wa tani 2,730 za  mahitaji halisi ya dawa za unga na viatilifu vya dawa ya maji lita 58,312 ambavyo vilihitajika kwa msimu wa mwaka huu .

Akizungumza kwa niaba ya viongozi wa AMCOS, Mwenyekiti wa Chama cha Msingi Mlingoti Mashariki, Said Makochela, alisema wao wanafuata taratibu na maelekezo yaliyotolewa na viongozi wa serikali na chama kikuu ikiwa ni pamoja na kuita majina ya wakulima ambao huuza korosho zao katika maeneo yao wakiwa wanawashirikisha maofisa ugani.

Alisema  kumekuwapo na vijana kutoka vijiweni ambao wamekuwa wakifika kwenye maeneo ya kugawa viuatilifu na kufanya fujo, kupora dawa.

Alisema mgawo wao umezingatia uzalishaji kwenye vituo 11 vya kukusanyia mazao vilivyopo katika vijiji vya Nandembo,  Tuleane, Kidugalo, Mkwajuni, Nandembo, Kangomba, Mmasonya, Mamboleo, Nambalapi, Lelolelo na Ngalinje.