Wakulima Manyara walia na magugu, “Kantangaze”

20Nov 2019
Daniel Sabuni
Hanang
Nipashe
Wakulima Manyara walia na magugu, “Kantangaze”

MAGUGU vamizi yanayofahamika kwa jina la Kitaalamu kama “Mauritus Thorns” yamevamia hekta 327 katika Kata ya Endasiwold wilaya ya Hanang mkoani Manyara na kuathiri ukuaji na uvunaji wa mazao mbalimbali.

“Kantangaze”.

Zaidi ya Gugu hilo, pia ugonjwa wa nyanya unaofahamika jina maarufu la  “Kantangaze” kitaalam “Tuta Absoluta” umevamia zaidi ya ekari 20 katika eneo la umwagiliaji la Garbapi, kwenye kata hiyo.

Diwani wa Kata ya Endasiwold, John Farayo aliyasema hayo jana katika ofisi ya Idara ya Maji ya Wilaya ya Hanang (RUWASA) akizungumza na Nipashe juu ya visumbufu vya mazao.

Bila kusema athari iko kiasi gani, Farayo alisema magugu hayo yamevamia na kuleta usumbufu kwa wakulima wa mazao ya jamii ya kunde ya ngwara, dengu, mbaazi na mahindi, kwa kuvyonza rutuba za mazao na hivyo kusababisha mazao kuwa machache na gharama za kuyakata kuwa kubwa.

“Nitafuatilia nikujulishe athari za kiasi cha mavuno yanavyotokea kutokana na gugu hilo, lakini tabia ya gugu hili unapolikata linamea haraka sana na hata wakati wa mavuno linaleta gharama kwani lazima ukodishe vibarua ili walikate na kutoa mazao yaliyopo shambani”alisema.

Alisema janga hilo watalifikisha kwenye uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ili wawaze kupata msaada wa kitaalamu na kuangamiza gugu hilo ambalo alisema lisipopatiwa ufumbuzi litaleta athari za kiuchumi kwa maana ya mavuno machache na kipato duni.

Aidha alisema katika eneo la umwagiliaji la Garbapi lenye ekari 20 ugonjwa wa nyanya wa "Kantangaze" umekuwa tatizo kutokana na kuharibu nyanya na kuleta hasara kwa wakulima kwani kila kiatilifu wanachotumia kimekuwa kikishindwa kumuangamiza mdudu huyo.

“Mdudu huyu anavizia nyanya zimestawi vizuri na inapofikia hatua ya kuzaa matunda huvamia na kuziathiri na kuozesha, hapa napo tunaomba msaada wa wataalamu ili tulime kwa usalama na kujenga uchumi wa Taifa letu”alisema Farayo.

Hivi karibuni, Mtafiti Dk. Never Zekaya kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela (NM-AIST), aligundua kiuatilifu alichokiita VURUGA cha kudhibiti mdudu mharibifu wa zao la mboga mboga kama nyanya na nafaka shambani, anayefahamika kwa jina maarufu la “Kantangaze”.

Vilevile mtaalamu wa kutoka Tasisi ya Kutafiti Viatilifu ya (TPRI) ya Kiropiki, ambaye ni mtafiti Mwandamizi, Maneno Chindege, alisema mdudu anayefahamika kama kiwavijeshi, kwa lugha ya kingereza “Armyworm” kwa jina la kitaalamu “Spodoptera frugipedra”, amevamia sehemu nyingi za Nchi hasa kwenye zao la mahindi.

Alisema kwa mujibu wa tafiti zilizofanyika Mwaka huu mwanzoni, kwa ushirikiano wa timu kutoka Wizara ya Kilimo, TARI, Chuo kikuu cha Sokoine (SUA) na TPRI, chini ya ufadhili wa Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa la (FAO) zimeonyesha kuwa endapo Nchi za Kusini mwa jangwa la Sahara na Nchi za SADC, wakulima wasipopata maelekezovizuri uwezekano wa kupoteza mavuno kati ya asilimia 29 hadi 52 unaweza kutokea.

“Baadhi ya mashamba ambayo tumeyatembelea na kukuta mdudu huyo amevamia wamepoteza mavuno kwa asilimia 100 ”alisema Chindege.

Alisema pia madhara mengine ni athari kwenye afya ya mimea kutokana na wakulima kuchanganya sumu mbali mbali kudhibiti kiwavi ambapo puche za mhindi hupata mabaka mabaka.

Alisema athari hiyo waliikuta katika eneo la Darera Wilayani Babati, Mkoani Manyara.Alisema wakulima hupata hasara kutokana na kupuliza dawa zaidi ya mara tano wakipambana na kiwavi jeshi hali inayopelekea kupata hasarakutokana na kutumia gharama kubwa kwenye madawa.

Alisema wakulima wengi wanatumia viatilifu bila kuzingatia maelekezo ya wataalam na hivyo kumfanya mdudu huyo kujenga usugu ambao hata ukimpulizia dawa hadhuriki.

Alitoa wito kwa wakulima kote nchini kutumia viatilifu vya MGUSO na endapo kiwavijeshi atakuwa ameingia katikati ya shinda la mmea wa mahindi watumie viuatilifu vya MFUMO.

“Ni kama Mwili wa binadamu, ni kama mtu anaumwa kwenye mguu lakini anameza Paracetamol halafu ukaona kwenye kisigino pamepona ina maana dawa hiyo imepita kwenye mfumo wa mwili,hivyo hivyo viatilifu vya mfumo hata kama mdudu amejificha dawa ikiingia kwenye mfumo wa mmea itamuangamiza popote alipo.

Chindege alisema viatilifu vya Mguso vimeandikwa “CONTACT INSECTICIDE” na vile  vya Mfumo vinaitwa “SYSTEMIC INSECTICIDE.

Habari Kubwa