Wakulima waangua kilio mbele ya Waziri Nchemba

05Jan 2017
Ashton Balaigwa
Morogoro
Nipashe
Wakulima waangua kilio mbele ya Waziri Nchemba

BAADHI ya wakulima katika Kata ya Tindiga, wilayani Kilosa,wamejikuta wakiangua kilio mbele ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Mwigulu Nchemba,kuelezea jinsi wanavyonyanyaswa na wafugaji ikiwamo kupigwa wanapofukuza mifugo kwenye mashamba yao.

Walimlalamikia kuwa wanapofikisha masuala yao kituo cha polisi, wafugaji hawachukuliwi hatua zozote kwa madai wamekuwa wakitoa fedha kwa baadhi ya askari polisi na kutoa mwanya kwa wafugaji hao kuendelea kuwapa vitisho.

Akiwasilisha malalamiko hayo huku machozi yamkimtiririka kwa Waziri Nchemba aliyetembelea kijiji hicho,mmoja wa wazee wa kijiji hicho,Omary Lupora,alisema watu sita wameshafariki kutokana na vitendo vya wafugaji kulisha mifugo yao katika mashamba ya wakulima na wanapowafukuza huambulia vipigo na kuchomwa sime na mishale.

“Waziri Mwigulu,sisi wengine ni wazee vitendo vinavyofanywa na wafugaji ni vya kinyama,wanaingiza mifugo yao kwa makusudi katika mashamba yetu sisi wakulima,tukifukuza ng’ombe ni vipigo vya fimbo wanazotembea nazo pamoja na kuchomwa sime,tayari watu sita wameshafariki katika kijiji hiki tunaomba utusaidie,” alisema Lupora.

Alisema hata Mkuu wa wilaya hiyo aliyeteuliwa hivi karibuni, hatoweza kudumu kwakuwa wafugaji hao wamekuwa tishio kubwa na kusababisha kuzuka kwa machafuko huku baadhi ya askari polisi wakiwalinda.

Naye Said Kimamba,alisema wamekuwa wakiishi kama wakimbizi ndani ya ardhi yao,kutokana na vitendo hivyo vya wafugaji kuwapiga na kulishia kwenye mashamba yao.

“Waziri wetu wewe ndio msaada pekee wa kutuokoa katika janga hili,tunanyanyaswa sana na wafugaji tumeshawasilisha kwa viongozi wakiwamo wa wilaya hadi mkoa, lakini hakuna hatua zozote zinazochukuliwa mpaka sasa,” alilalamika na kuangulia kilio.

Mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo(Chadema), Joseph Haule,alisema baadhi ya wananchi wa kijiji hicho, wanalazimika kulala juu ya miti nyakati za usiku wakihofia kuvamiwa na wafugaji baada ya kufukuza ng’ombe katika mashamba yao.

Waziri Mwigulu,aliwaahidi wananchi hao,kuongeza vitendea kazi ikiwamo magari na pikipiki na kuongeza idadi ya askari ili kufika haraka katika matukio na kuahidi kuwachukulia hatua kali askari yeyote atakayebainika kufanya ushirika wa karibu na wafugaji wanaofanya vitendo vya uhalifu.

Habari Kubwa