Wakulima wadogo waitiwa vikundi

20Feb 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Wakulima wadogo waitiwa vikundi

WAKULIMA wadogo katika mikoa 10, wametakiwa kujiunga kwenye vikundi ili kupata urahisi wa kuwezeshwa kubadili mfumo wa maisha kupitia kilimo.

Wito huo ulitolewa na Katibu Mtendaji wa Mfuko Kichochezi wa Kuendeleza Kilimo Biashara Ukanda wa Kusini mwa Tanzania, Dk. John Kyaruzi, alipokuwa akizungumza na waandishi jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Dk. Kyaruzi alisema zipo fursa nyingi kwa wakulima wadogo wanaojiunga katika vikundi.

Alisema ili kubadili mfumo na kilimo kuwa cha biashara, lazima kuwapo na mazao ya kutosha yenye ubora, miundombinu mizuri ikiwamo barabara na upatikanaji wa maji ya uhakika kwa mwaka mzima.

“Mkulima mdogo ana changamoto nyingi ikiwamo ukosefu wa mtaji, mbolea, dawa za kuua wadudu shambani, mbinu bora za kuhifadhi mazao kabla ya kuyauza, vifaa bora vya kisasa pamoja na uhakika wa soko. Yote haya yapo chini ya uwezo wetu, tunachotaka wakulima wajiunge na wapeleke malalamiko yao kwa kampuni au taasisi moja ambayo tutaitumia kutatua matatizo yao.

Alisema kwa mfano, wakulima wa miwa Morogoro au Kagera, wakilalamika ubovu wa barabara watazungumza na Kiwanda cha Sukari Mtibwa au cha Kagera watengeneze barabara hiyo kisha watawapelekea mchanganuo walipwe," alisema.

Kwa upande wa wakulima alisema wakilalamika ukosefu wa pembejeo, watazungumza na kampuni inayosambaza pembejeo watoe huduma hiyo halafu wao watalipa gharama zote.

“Tunachotaka ni kumaliza changamoto zinazomfanya mkulima kushindwa kutoa mazao bora na mengi, kwa kawaida soko linataka kitu kilicho bora kwa idadi kubwa. Kiwanda cha nyanya kinaweza kuhitaji tani 1,000 kwa siku, lakini wakulima katika mkoa husika uwezo wao ni kulima nusu yake, lazima mwekezaji ataagiza bidhaa hiyo nje ya nchi kwani sisi tunataka kuondoa hilo,” alisema Dk. Kyaruzi.

Akizungumzia matatizo ya kukopesha wakulima, Dk. Kyaruzi alisema huo si uamuzi sahihi kwa sababu kumkopesha maana yake ni kumfunga mkulima asiwe huru kwa kile anachofanya akifikiria namna ya kurudisha fedha alizokopa.

“Wakulima wadogo wana matatizo mengi ya kifedha, mkopo hauwezi kuwa suluhisho la matatizo yao zaidi ya kuongeza matatizo, unaweza kumpa mkopo mkulima akaanza kutatua matatizo ya nyumbani ikiwamo afya au sare za shule za mtoto wake, hadi akianza kulima, fedha zote kamaliza kwenye matatizo ya kifamilia, tukasema mbinu hii si muafaka,” alisema Dk. Kyaruzi.
Kwa sasa mfuko huo unasaidia wakulima katika mikoa 10.

Mikoa hiyo ni Dar es Salaam, Morogoro, Pwani, Dodoma na Singida. Mikoa mingine ni Rukwa, Njombe, Iringa, Songwe, Mbeya na Rukwa, ambapo mfuko huo huchochea ongezeko la viwanda katika maeneo hayo kulingana na aina ya mazao yanayolimwa ikiwamo matunda, mboga, nafaka na mifugo.

Mfuko huu ulianzishwa mwaka 2010 kati ya wabia wa kilimo ikiwamo Serikali ya Tanzania, wakulima wadogo, wawekezaji wa ndani na nje pamoja na balozi kutoka mataifa mbalimbali yenye uwakilishi wake hapa nchini.

Lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo ni kuhakikisha wakulima wanaondokana na changamoto zinazowafanya kukosa soko la uhakika na mazao bora yatakayoleta ushindani katika Soko la Kimataifa.

Habari Kubwa