Wakulima wapongeza bei ya Pamba kuongezeka

11Jun 2021
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Wakulima wapongeza bei ya Pamba kuongezeka

WAKULIMA wa zao la Pamba hapa nchini wamepongeza bei ya Pamba kuongezeka katika msimu wa mwaka huu, kutoka Sh. 810 mwaka Jana hadi 1,050.

Kaimu mrajisi wa vyama vya ushirika mkoani Shinyanga Hilda Boniphace, akizungumza kwenye kikao hicho cha zao la Pamba.

 

Wakulima wametoa pongezi hizo leo, kwenye kikao cha umoja wa vyama vya ushirika cha kilimo cha zao la Pamba hapa nchini TANCCOPs. kilichofanyika katika ukumbi wa chama kikuu cha ushirika mkoani Shinyanga SHIRECU.

Mmoja wa wakulima wa zao hilo la Pamba Joseph Kinyerero kutoka Mbongwe mkoani Geita ,alisema amefarijika sana bei ya Pamba kuongezeka, hali ambayo itawainua wakulima kiuchumi.

Mwenyekiti Mwanzilishi wa umoja huo wa vyama vya ushirika wa kilimo cha zao la Pamba Benjamini Mikomangwa, akisoma taarifa yake kwa wajumbe, alisema wamepigania sana ongezeko hilo la bei ya Pamba.

Amesema awali wafanyabiashara kutoka makampuni binafsi, katika msimu wa ununuzi wa zao la Pamba mwaka huu, walitaka bei iwe shilingi 940, lakini wao wakapigania hadi kufika Shilingi hiyo 1,050.

Naye Meneja wa chama kikuu cha ushirika kutoka mkoani Geita Venance musiba, akisoma mipango mikakati ya umoja huo, alisema malengo yao kuanzia 2021-2024, ni kuhakikisha wakulima wa Pamba wanapata Pembejeo zenye ubora na kwa wakati, pamoja na vyama vya msingi vya ushirika Amcos kuwa na mizani imara.

Kwa upande wake Kaimu mrajisi wa vyama vya ushirika mkoani Shinyanga Hilda Boniphace, aliutaka umoja huo wawe pia na mashamba darasa ya kilimo cha zao la Pamba, ili wakulima wapate somo kwa vitendo kwenye mashamba hayo na kuongeza uzalishaji.

Aidha kikao hicho kimeshirikisha wajumbe kutoka mikoa yote ambayo inalima zao la Pamba hapa nchini, ikiwamo Singida, Simiyu, Mpanda, Tabora, Geita, Mwanza, pamoja na Shinyanga. 

Habari Kubwa