Wakurugenzi h’shauri kuwekwa kikaangoni

26May 2020
Gwamaka Alipipi
Dodoma
Nipashe
Wakurugenzi h’shauri kuwekwa kikaangoni

BUNGE la 11 linatarajia kuendelea leo, ambapo pamoja na mambo mengine, wakurugenzi wa halmashauri waliotajwa kufuja fedha katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wanatarajiwa kujadiliwa wiki hii.

Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, leo wabunge wataendelea kuchangia taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu taarifa za ukaguzi za CAG kwa hesabu zilizokaguliwa za serikali na mashirika ya umma kwa mwaka 2018/19.

Kesho, Bunge litaanza kujadili ripoti kuu ya mamlaka ya serikali za mitaa, iliyowasilishwa na CAG, baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), kuwasilisha taarifa za mkaguzi huyo, ikifuatiwa na wabunge kuijadili ripoti hiyo, serikali kujibu hoja za kamati pamoja na wenyeviti kuhitimisha siku hiyo hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti ya CAG 2018/19 iliyowasilishwa kwenye Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), ilibaini viashiria vya ubadhirifu wa Sh. bilioni 1.247 uliofanywa na halmashauri 12.

Kwenye ripoti hiyo, CAG alieleza kuwa: “Serikali Kuu inapaswa kuchukua hatua dhidi ya halmashauri hizo. Uwapo wa udanganyifu huu ni ishara kuwa mamlaka za serikali za mitaa husika zinakosa utaratibu sahihi wa kubaini udanganyifu kabla haujatokea kwa kutokuwa na mifumo ya udhibiti wa ndani inayofanya kazi ipasavyo.”

Vilevile, katika ripoti hiyo CAG alieleza kuwa kati ya hesabu za mwisho za halmashauri 185 zilizokaguliwa, halmashauri 176 (asilimia 95) zilipata hati inayoridhisha, halmashauri 9 (asilimia 5) zilipata hati yenye shaka.

Alieleza kuwa ingawa baadhi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa zimepata hati inayoridhisha, mamlaka hizo zilibainika kuwa na upungufu kutokana na kushindwa kufuata maagizo ya Bunge, sheria, kanuni, sera za serikali, na miongozo mbalimbali.

Aidha, CAG alibaini kuwa mamlaka za serikali za mitaa 74 zilifanya manunuzi ambayo hayakushindanisha wazabuni yenye thamani ya Sh. bilioni 32.461, bila kuwa na sababu zilizojitosheleza.

Pia, alibaini kuwa mamlaka za serikali za mitaa 47 zilifanya manunuzi yenye thamani ya Sh. bilioni 9.234 ambayo hayakupitishwa na bodi za zabuni, Mamlaka za serikali za mitaa 34 zilifanya manunuzi yenye thamani ya Sh. bilioni 4.353 kutoka kwa wazabuni ambao hawakuidhinishwa.

Vilevile, CAG alieleza kuwa mamlaka za serikali za mitaa 39 zilifanya manunuzi yenye kiasi cha Sh. bilioni 1.476 kwa kutumia masurufu, Mamlaka za Serikali za Mitaa 43 zilinunua na kupokea bidhaa zenye thamani ya Sh. bilioni tano bila kukaguliwa na kamati za ukaguzi na upokeaji wa bidhaa.

Habari Kubwa