Wakurugenzi sita watumbuliwa HESLB

14Jun 2018
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wakurugenzi sita watumbuliwa HESLB

WAKURUGENZI sita wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), wameachishwa kazi kwa makosa mbalimbali ikiwamo uzembe na kuisababishia serikali hasara ya Sh. bilioni 21.3.

Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru.

Wakurugenzi hao ni Mkurugenzi wa Urejeshaji wa Mikopo, Juma Chagonja, Mkurugenzi wa Upangaji na Ugawaji Mikopo, Onesmus Laizer na Mkurugenzi Msaidizi wa Ugawaji Mikopo, John Elias.

Wengine ni Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo, Robert Kibona, Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani, Heri Sago na Mkurugenzi Msaidizi wa Upangaji Mikopo, Chikira Jahari.

Taarifa hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa bodi hiyo, Abdul-Razaq Badru, Alipozungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya HESLB.

Badru alisema uamuzi wa kuwaachisha kazi wakurugenzi hao ulifikiwa juzi na bodi ya wakurugenzi baada ya kupitia taarifa zao.

Badru alisema wakurugenzi hao walisimamishwa kazi kati ya 2016 na mwaka jana kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali zilizowakabili.

Alisema watumishi hao walikuwa wanakabiliwa na tuhuma ikiwamo uzembe uliokithiri, kushindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo kwa mujibu wa Sheria ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2002 na kanuni zake na kusababisha hasara ya upotevu wa fedha za serikali.

"Kama sheria na kanuni za utumishi wa umma zinavyotaka, baada ya taratibu za ndani kukamilika Februari mwaka huu, bodi ya wakurugenzi iliunda kamati ya uchunguzi inayowajumuisha wataalamu wa sheria, fedha na utumishi wa umma kwa lengo la kufanya uchunguzi na mahojiano na watuhumiwa hao," alisema Badru.

Alisema kamati hiyo imefanya kazi kwa kuwasilisha taarifa kwa bodi ya wakurugenzi kwa ajili ya maamuzi, baada ya uchunguzi uliofanywa na kamati na utetezi uliotolewa na watumishi hao.

Alisema bodi ya wakurugenzi imejiridhisha kuwa watumishi hao walitenda makosa ya kinidhamu na hivyo wanastahili adhabu kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazosimamia utumishi wa umma.

Akiainisha makosa yao, mkurugenzi mkuu wa HESLB alisema Mkurugenzi wa Urejeshaji Mikopo Chagonja ameachishwa kazi kwa kushindwa kutekeleza majukumu yake ya urejeshaji wa mikopo kwa mujibu wa kanuni na taratibu za urejeshaji wa mikopo hiyo; pamoja na kufanya uzembe uliokithiri na kusababisha hasara kwa serikali.

Alisema Mkurugenzi wa Upangaji na Ugawaji Mikopo Laizer amekutwa na makosa matatu, ikiwamo kushindwa kutekeleza majukumu yake ya utoaji wa mikopo kwa mujibu wa kanuni na taratibu za utoaji wa mikopo.

"Pia amesababisha uzembe uliosababisha hasara ya Sh. bilioni 7.1 kwa serikali na kufanya uzembe uliokithiri," alisema Badru.

Badru alisema Mkurugenzi Msaidizi wa Ugawaji wa Mikopo Elias alikutwa na makosa matatu ya kushindwa kutekeleza majukumu yake ya utoaji wa mikopo kwa mujibu wa kanuni na taratibu za utoaji wa mikopo, kufanya uzembe uliosababisha hasara ya Sh. bilioni 7.1 na kufanya uzembe uliokithiri.

Aidha, alisema Mkurugenzi Msaidizi wa Urejeshaji Mikopo Kibona ameachishwa kazi kwa makosa matatu ya kushindwa kutekeleza majukumu yake ya urejeshaji wa mikopo kwa mujibu wa kanuni na taratibu za urejeshaji wa mikopo, uzembe uliosababisha hasara kwa serikali na kufanya uzembe uliokithiri.

Alisema kwa upande wa Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani Sago, yeye alishindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo kama Mkaguzi Mkuu kwa kushindwa kuibua vitendo viovu vilivyokuwa vikiendelea.

Badru alisema Mkurugenzi Msaidizi wa Upangaji Mikopo Jahari ameachishwa kazi kwa makosa mawili: Kufanya uzembe uliosababisha hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 7.1 kwa serikali na kufanya uzembe uliokithiri.

Aidha, alisema wahusika wote wameandikiwa barua kuhusu uamuzi huo na wamepewa taarifa kwamba wana haki ya kukata rufani kwa Tume ya Utumishi wa Umma ndani ya siku 45, endapo hawakuridhika na uamuzi wa bodi ya wakurugenzi.

Pia bodi ya wakurugenzi imewataka watumishi wote wa HESLB kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo halali iliyotolewa.

Alisema watumishi wa bodi pia wanapaswa kuzingatia uadilifu na umakini ili kuepuka vitendo vinavyoweza kuisababishia hasara serikali.

Naye Mkurugenzi wa Sheria wa HESLB, Abdallah Mtibora, alisema watapeleka taarifa kwa mamlaka nyingine zinazohusika na uchunguzi ili zichukue hatua kwa mujibu wa sheria.

 

WANAFUNZI 122,000

Februari 16, 2016 Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Prof. Joyce Ndalichako alisitisha mkataba wa ajira wa Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo, George Nyatega pamoja na kuwasimamisha kazi wakurugenzi watatu kati ya hao sita.

HESLB inataraji kutoa mikopo kwa jumla ya wanufaika 122,000 kwa mwaka huu wa masomo.

Kati ya wanafunzi hao, wapya ni 40,000 na wanaoendelea na masomo vyuoni ni zaidi ya wanufaika 80,000.

Katika wanafunzi wapya, wanawake ni 14,000 sawa na asilimia 35 na wanaume ni 26,000 sawa na asilimia 65.

Kwa mwaka huu, idadi ya wanufaika wapya wa mikopo imeongezeka ikilinganishwa na mwaka jana ambako walikuwa 33,000.

Katika bajeti ya fedha za mikopo kwa mwaka 2018/19, jumla ya Sh. bilioni 427 zimetengwa ili kufanikisha suala hilo.

Katika mikopo hiyo, HESLB inatoa kipaumbele kwa waombaji mikopo waliodahiliwa katika kozi zinazohitajika kuchochea ukuaji wa uchumi wa viwanda kama uhandisi wa aina zote, kozi ya sayansi ya kilimo na wanyama na kozi zinazohusiana na gesi na nishati.

Shirika la Posta lina vituo 180 nchini kote vinavyotoa huduma kwa wanafunzi wanaoomba mikopo hiyo.

 

* Imeandikwa na Beatrice Shayo, Gloria Katunzi TSJ

 

Habari Kubwa